West Ham wamtwaa beki Kurt Zouma kutoka Chelsea kwa Sh3.9 bilioni

West Ham wamtwaa beki Kurt Zouma kutoka Chelsea kwa Sh3.9 bilioni

Na MASHIRIKA

WEST Ham United wamemsajili beki matata wa Chelsea, Kurt Zouma, 26, kwa Sh3.9 bilioni.

Kocha David Moyes amekuwa na kiu ya kuimarisha safu yake ya ulinzi kadri anavyolenga kuendeleza matokeo bora yaliyosajiliwa na kikosi chake kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu uliopita wa 2020-21.

West Ham pia wanashiriki kipute cha Europa League na wametiwa katika Kundi H kwa pamoja na Dinamo Zagreb, Genk na Rapid Vienna.

Zouma ambaye ni raia wa Ufaransa, alichezea jumla ya mechi 36 mnamo 2020-21 na kuondoka kwake kutamchochea kocha Thomas Tuchel kumsajili difenda mwingine raia wa Ufaransa, Jules Kounde wa Sevilla.

Zouma alijiunga na Chelsea akiwa na umri wa miaka 19 baada ya kuagana na Saint-Etienne ya Ufaransa mnamo Januari 2014. Amewahi pia kuvalia jezi za Stoke City na Everton kwa mkopo. Kufikia sasa, amewajibishwa na Chelsea katika jumla ya mechi 151 na akafunga jumla ya mabao 10 katika mashindano yote.

West Ham wameanza kampeni za EPL msimu huu kwa matao ya juu baada ya kupiga Newcastle United (4-2) na Leicester City (4-1) katika michuano miwili ya kwanza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kenya, Uholanzi kwenye ushirikiano wa kuboresha kilimo cha...

Manchester City wazidisha masaibu ya Arsenal katika EPL