West Ham wasajili kipa matata wa PSG, Alphonse Areola, kwa mkataba wa miaka mitano

West Ham wasajili kipa matata wa PSG, Alphonse Areola, kwa mkataba wa miaka mitano

Na MASHIRIKA

WEST Ham United wameimarisha zaidi safu yao ya ulinzi kwa kumsajili kipa mzoefu wa Paris Saint-Germain (PSG), Alphonse Areola.

Areola, 29, amepokezwa mkataba wa miaka mitano ugani London Stadium baada ya kuridhisha zaidi vinara wa West Ham waliojivuni huduma zake kwa mkopo mnamo 2021-22.

Anakuwa mchezaji wa pili kuingia katika sajili rasmi ya West Ham ambao pia wamejinasia maarifa ya beki matata raia wa Morocco, Nayef Aguerd kutoka Rennes ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Ingawa West Ham wanaovizia pia kiungo mvamizi Jesse Lingard kutoka Manchester United hawajafichua fedha walizoweka mezani kwa ajili ya Areola, inaaminika kwamba walishawishi kipa huyo kusalia uwanjani London Stadium kwa Sh1.6 bilioni.

Areola aliwajibishwa na West Ham mara 18 mnamo 2021-22 katika mashindano manne tofauti – Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Europa League, FA Cup na Carabao Cup. Anatarajiwa sasa kukabiliana na ushindani mkali kutoka kwa kipa Lukasz Fabianski, 37, kupigania nafasi ya kuwajibikia kikosi cha kwanza cha West Ham mara kwa mara. Fabianski ambaye pia amewahi kudakia Arsenal, alirefusha mkataba wake kambini mwa West Ham kwa mwaka mmoja zaidi mnamo Mei 2022.

West Ham ambao sasa wanashiriki mazoezi nchini Scotland, watafahamu washindani wao kwenye mchujo wa kipute kipya cha Europa Conference League mnamo Agosti 1, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Rooney kurudi shule kusomea ukocha baada ya kuondoka Derby...

KIDIJITALI: Apu ya ‘Kalro Garlic’ kusaidia wakulima...

T L