Michezo

Western Stima yaondoa hofu licha ya klabu kadhaa kumezea mate masogora wake

July 3rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Western Stima kipo katika hatari ya kuagana na wanasoka wao wa haiba kubwa kutokana na uchechefu wa fedha ambao umechangiwa na hatua ya kampuni ya Kenya Power kusitisha udhamini wao.

Vikosi vingi vya haiba katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) sasa vinamezea mate masogora wa Stima walioridhisha zaidi katika kampeni za msimu uliopita kwa matumaini ya kuchuma nafuu kutokana na hali mbovu ya kifedha ya waajiri wao na hatimaye kuwasajili.

Kati ya wachezaji wanaotarajiwa kukatiza uhusiano wao na Stima ni Kelly Wesonga, Fidel Origa, Maurice Ojwang na mfumaji chipukizi wa Harambee Stars, Benson Omalla.

Ingawa hivyo, mwenyekiti Laban Jobita amesisitiza kwamba uthabiti wao hautayumbishwa na tukio hilo kwa kuwa wanapania kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho baada ya muhula wa usajili wa wachezaji kufunguliwa rasmi.

“Tuna mpango wa kujinasia maarifa ya chipukizi wengi watakaoongoza kampeni zetu zijazo. Stima haitamkwamilia mchezaji yeyote anayeazimia kutafita hifadhi mpya kwingineko,” akatanguliza kinara huyo kwa kusisitiza haja ya klabu zinazovizia wanasoka wa Stima kuzingatia taratibu zilizopo za kusajili wachezaji.

“Wote wanaotaka kuagana nasi wako huru kufanya hivyo ila kwa kuzingatia taratibu zote zilizopo. Sera zetu haziwezi kuturuhusu kumkwamilia mchezaji ambaye anahisi atapiga hatua kubwa kitaaluma akivalia jezi za kikosi kingine ispokuwa Stima,” akasema Jobita.

Jobita ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Gor Mahia na Kisumu Hotstars, amefichua kuwa mikakati ya Stima kwa sasa ni kutafuta mdhamini mpya na kutathmini maombi ya wanasoka wengi wanaotazamia kujiunga nao kabla ya kuanza mchakato wa kusajili wanafunzi wa shule za upili na vyuo kwa minajili ya msimu ujao wa KPL.