Habari Mseto

Westgate: Korti yasema washukiwa wana kesi ya kujibu

January 15th, 2019 2 min read

Na Richard Munguti

MAHAKAMA imewapata watu watatu walioshtakiwa kwa shambulizi la kigaidi katika jengo la kibiashara la Westgate Mall, eneo la Westlands, Nairobi lililosababisha vifo vya watu 67, kuwa na kesi ya kujibu huku mwenzao mmoja akiachiliwa huru.

Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani, Nairobi Bw Francis Andayi, alisema watatu hao wana kesi ya kujibu.

“Ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka umewahusisha washtakiwa hao watatu na shambulizi hilo lililosababisha hofu kuu na mshtuko kwa wananchi wa Kenya na raia wa kigeni,” alisema.

Hakimu huyo alisema washtakiwa hao watapewa fursa ya kujitetea kwamba “ndio waliohusika na shambulizi hilo lililosababisha maafa makubwa.”

“Baada ya kuchambua ushahidi wote uliowasillishwa na mashahidi zaidi ya 30 nimefikia uamuzi kwamba mlihusika na shambulizi hilo katika jengo la kibiashara la Westgate Mall,” aliamua Bw Andayi.

Hakimu huyo aliwaeleza washtakiwa kuwa watapewa fursa ya kujitetea kabla ya adhabu kutolewa.

Shambulizi hilo lilitekelezwa miaka sita iliyopita liliangamiza wafanyabiashara na watu wengine waliokuwa hapo.Watu zaidi ya 100 pia walisalia wakiuguza majeraha.

Waliopatikana na kesi ya kujibu ni Mabw Ahmed Abdi, Liban Omar na Hussein Mustafa.

Bw Andayi alimwachilia huru mshukiwa wa nne Bw Adan Dheg.

Wote wanne walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la kutekeleza shambulizi la kigaidi mnamo Septemba 21 2013.Kesi hiyo ilianza kusikizwa mnamo Januari 15, 2014.

Wanne hao walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la kufanya njama za kutekeleza tendo la kigaidi.Pia walikabiliwa na shtaka la kusababisha mauaji ya watu 67 walipotekeleza shambulizi hilo.

Kundi la Al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia lilidai kuhusika na shambulizi hilo.

Kesi hiyo itatajwa Januari 21 ndipo watengewe siku ya kuanza kujitetea katika kesi hiyo ambayo wakipatikana na hatia watahukumiwa kifungo cha maisha.

Wakati huo huo, katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) kesi ya sakata iliyokumba shirika la kitaifa la Huduma kwa Vijana (NYS) ilianza kusikizwa.

Hakimu mwandamizi, Bw Peter Ooko alifahamishwa kuwa aliyekuwa katibu mkuu wizara ya ugatuzi, Bi Lillian Omollo, aliyekuwa mkurugenzi mkuu Richard Ndubai na washukiwa wengine 30 walihusika na ufujaji wa zaidi ya Sh60 milioni.

Kiongozi wa mashtaka Bi Verah Amisi alimweleza hakimu mwandamizi Bw Ooko Sh8bilioni zilipotea katika kashfa zilizokumba shirika hilo la NYS.

Korti ilijulishwa baadhi ya mashahidi walikuwa wameshtakiwa na washukiwa hao.

“Katika kesi ya sasa dhidi ya washukiwa hawa 33, upande wa mashtaka utawasilisha ushahidi kuthibitisha jinsi kila mmoja alivyohusika na ulaghai wa pesa hizo.

Mahakama ilifahamishwa kuwa pesa zilitoweka kutoka shirika la NYS kwa njia ya udanganyifu hukukampuni kadhaa zikihusika na utoaji huduma feki na kulipwa mamilioni ya pesa.

Mahakama ilielezwa kuwa mamilioni ya pesa za umma zilitoweka kupitia malipo kwa bidhaa ambazo hazikuwa zimewasilishwa kwa NYS.

Akianza kutoa ushahidi mkurugenzi wa idara ya ununuzi wa bidhaaa za umma, Bi Joyce Namisi Ala, alisema uchunguzi katika NYS ulibaini kuwa bidhaa hazikuuzwa na kampuni zilidai malipo.Kesi inaendelea leo