Weta aamua ni Lusaka tosha ugavana 2022

Weta aamua ni Lusaka tosha ugavana 2022

Na BRIAN OJAMAA

KIONGOZI wa Ford Kenya Moses Wetang’ula amemwidhinisha rasmi Spika wa Seneti Ken Lusaka kuwania ugavana wa Bungoma katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Uungwaji mkono wa Seneta huyo wa Bungoma unajiri siku chache baada ya mbunge wa Kimilili Didmus Wekesa Barasa kushabikia azma ya Lusaka kuwania kiti hicho.

Wetang’ula, ambaye ni Seneta wa Bungoma, alitoa wito kwa wakazi kumwangusha gavana Wycliffe Wangamati katika uchaguzi mkuu ujao akisema amefeli kutimiza ahadi alizotoa kwa wananchi 2017.

Alisema Wangamati hajatekeleza miradi yoyote ya maendeleo katika miaka minne iliyopita licha ya Bungoma kupokea mabilioni ya fedha kutoka kwa Serikali Kuu.

Bw Wetang’ula alisema hayo Jumamosi alipofanya mkutano wa mashauriano nyumbani kwa diwani Elizabethi Tindi, katika kijiji cha Mabusi, eneobunge la Tongaren.

Alielezea matumaini kuwa Spika Lusaka atawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Ford Kenya.

“Tulimleta Wangamati tukidhani kuwa ataleta maendeleo katika kaunti hii, lakini ametuvunja moyo,” Bw Wetang’ula akasema.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alimkashifu Gavana Wangamati kwa kuendeleza ufisadi katika serikali ya kaunti ya Bungoma na hivyo kuwaacha wakazi wakiumia.

“Tulipomleta Wangamati kwenu wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017, watu wengi hawakumfahamu. Sasa amepata utajiri kutokana na pesa za walipa ushuru na kuanza kujigamba jinsi pesa zitakavyomwezesha kushinda tena. Atashangaa sana,” akasema Bw Wetang’ula.

Alimfananisha Wangamati na mchungaji ambaye hukama ng’ombe malishoni kiasi kwamba hurejesha ng’ombe nyumbani bila maziwa huku wengine wakiwa wamepotea.

Uhasama kati ya Wetang’ula na Wangamati ulianza mwaka 2020, wakati gavana huyo alishiriki katika njama ya kumpokonya wadhifa wa kinara wa Ford Kenya.

Wengine walioshiriki katika mapinduzi hayo ni mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi na mwenzake wa Tongaren Dkt Eseli Simiyu.

Wadadisi wanasema Gavana Wangamati atakuwa na wakati mgumu kudumisha kiti chake kutokana na upinzani mkali kutoka kwa Wetang’ula na Spika Lusaka.

Bw Lusaka ambaye alipoteza kiti cha ugavana wa Bungoma 2017 baada ya kushindwa na Bw Wangamati amethibitisha kuwa atawania wadhifa huo tena.

You can share this post!

Ngirici ataka wahudumu wa bodaboda kujiepusha na uhalifu

TAHARIRI: Tuonyeshe ukomavu wa demokrasia

T L