Siasa

Baada ya MaDVD, Weta naye asukumwa Ford K imezwe na UDA

Na SHABAN MAKOKHA June 21st, 2024 2 min read

BAADA ya chama cha Amani National Congress (ANC) kutangaza rasmi kuungana na United Democratic Alliance (UDA), shinikizo zinazidi kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kuvunja chama chake cha Ford Kenya.

ANC kinahusishwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi huku kiongozi wa UDA akiwa Rais William Ruto.

Vyama hivyo na Ford Kenya cha Wetangula, ni washirika katika Muungano tawala wa Kenya Kenya.

Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala amemtaka Bw Wetang’ula afuate nyayo za Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye amekubali kujiunga na UDA na kuvunja ANC.

Uongozi wa ANC mnamo Jumatano, Juni 19, 2024 ulikutana na Rais Ruto na kuamua kuwa chama hicho kitavunjwa na kujiunga na UDA.

Mkutano huo uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi, pia ulihudhuriwa na Bw Mudavadi na Issa Timammy ambaye ni Gavana wa Lamu.

“Ili nchi iwe na chama imara, lazima tuweke kando maringo na tukubali kufanya kazi pamoja. Hatuwezi kuwa na mwelekeo moja wa kisiasa kama tunaegemea vyama vyetu vidogo ilhali nchi inaongozwa na chama kikubwa,” akasema Bw Malala.

Seneta huyo wa zamani Kakamega alimpongeza Bw Mudavadi kwa kukubali kuvunja ANC na kujiunga na UDA akisema hilo litakuza umoja wa nchi.

Vyama kutumika kwa ajili ya uchaguzi

“Vyama vya kisiasa havifai kuwa vile vya kutumika tu wakati wa uchaguzi. Tunataka kuvigeuza vyama vya kisiasa kama asasi za kuhubiri amani na umoja wa nchi,” akaongeza Bw Malala.

Kando na Ford Kenya, alivitaka vyama vingine tanzu ndani ya Kenya Kwanza vifuate mkondo wa ANC na kujiunga na chama tawala, akisema hiyo itarahisishia kazi Rais William Ruto kwenye uchaguzi wa 2027.

Kiongozi huyo aliitaka jamii zinazoishi Magharibi mwa Kenya zijiunge na UDA ili zinufaikie miradi ya maendeleo.

“Nimesikia watu wakilalamika kuwa watu wa Bungoma wanapata miradi mingi ya maendeleo kuliko Kakamega. Hiyo ni kweli kwa sababu watu wa Bungoma walichangia kubuniwa kwa serikali hii,” akasema.

Bw Malala alisema kuwa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa uga wa Masinde Muliro na uwanja wa ndege wa Matulo unastahili kuwafungua macho wakazi wa kaunti za Kakamega, Vihiga na Busia kubadilisha jinsi wanavyopiga kura.

“Mapenzi yao kwa siasa za upinzani yanawaponza. Wabadilishe jinsi wanavyopiga kura na waanze kuunga miradi ya serikali,” akaongeza.

Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale

Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale alikuwa amemkashifu Bw Wetang’ula kwa kutumia wadhifa wake kuhakikisha kuwa miradi mingi ya serikali iliyotengewa Magharibi inaanzishwa Bungoma.

Bw Khalwale alilalamika kuwa Kakamega imetengwa katika utawala wa sasa ilhali ndiyo makao makuu ya jamii za Magharibi wala si Bungoma.

Hata hivyo, Bw Malala alisema kuwa Bungoma walifanya kazi nzuri kwa sababu ndio walimpigia Rais Ruto kura 2022.

“Njia pekee ambayo Waluhya watatumia kupata uongozi wa nchi hii ni kujiunga na chama kikubwa cha kisiasa na hiyo ni UDA,” akasema Bw Malala.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa watu kutoka Magharibi mwa nchi wamehadaiwa kwa miaka mingi kupitia vyama vidogo na lazima wagutuke na kuwekeza katika chama kikubwa ili serikali nayo iwathamini.