Habari Mseto

Wetang'ula aanza kujipigia debe mapema kumrithi Uhuru 2022

June 28th, 2020 1 min read

Na GERALD BWISA

KIONGOZI wa Chama cha Ford-Kenya, Bw Moses Wetang’ula ameanza kujipigia debe akimezea mate kiti cha urais 2022.

Seneta huyo wa Kaunti ya Bungoma alisema chama chake kiko imara na hakuna atakayemtishia ili akivunje.

Akizungumza katika eneo la Amagaro, Kaunti ya Trans-Nzoia alipohudhuria mazishi, Bw Wetang’ula alimkashifu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, akidai anapotosha jamii ya Waluhya.

“Wakati Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto waliingia mamlakani 2013 waliahidi kujenga barabara ya Kitale-Kapenguria ilhali bado iko vilevile. Tunaambiwa tujiunge na serikali ili tupate maendeleo Magharibi. Hilo haliwezekani,” akasema.

Alisisitiza: “Serikali pekee inayoweza kuleta maendeleo ni ile nitakayounda mwaka wa 2022. Ninaomba kila mmoja wenu ajiandikishe kupiga kura ili mnipe nafasi kuwa Rais wenu.”

Aliwalaumu pia Waziri Eugene Wamalwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, akisema wanadanganya wakazi kuwa wataleta maendeleo.