Wetang’ula achemka kusikia mgombea mwenza wa Ruto atatoka Mlima Kenya

Wetang’ula achemka kusikia mgombea mwenza wa Ruto atatoka Mlima Kenya

Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO kuhusu suala la uteuzi wa mgombeaji mwenza katika muungano wa Kenya Kwanza Jumanne, Machi 1, 2022 uliendelea kuvutia hisia za ziongoni wengine katika muungano huo. 

Siku moja baada ya chama cha Amani National Congress (ANC) chake Musalia Mudavadi kupuuzilia mbali kauli ya Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kudai mtu kutoka eneo la Mlima Kenya ndiye atateuliwa kwa wadhifa huo, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula sasa amechemka kuhusu suala hilo.

Kulingana na seneta huyo wa Bungoma, falsafa ya muungano huo haijajengwa katika misingi ya ugavi wa nyadhifa bali kufufua uchumi wa Wakenya.

“Mungano wa Kenya Kwanza hauongozwi na tamaa ya ugavi wa mamlaka bali huduma kwa Wakenya. Kwa mfano, unalenga kufufua na kuendeleza uchumi, kupunguza mzigo wa madeni, kuwasaidia wakulima wetu, kujenga taifa lenye usawa miongoni mwa mipango mingine yenye manufaa kwa wananchi wa tabaka la chini,” akasema kupitia ukurasa wake wa facebook.

Mnamo Jumatatu, Bw Gachagua ambaye ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto alisisitiza kuwa Dkt Ruto ndiye atapeperusha bendera ya Urais katika Kenya Kwanza na mgombea mwenza wake atatoka eneo la Mlima Kenya.

Akiongea katika runinga ya Citizen, Bw Gachagua alisema kuwa hatua ya Mudavadi na Wetang’ula kukubali kushirikiana na chama cha United Democratic Alliance (UDA), haikuvuruga mpangilio wao kuhusu suala hilo.

“Ninavyofahamu ni kwamba Ruto ndiye mgombea urais wa Kenya Kwanza na mgombeaji mwenza atateuliwa kutoka Mlima Kenya wakati ukitimu. Huo ndio mpangilio tuliokuwa nao kabla ya hawa marafiki zetu kuungana nasi, na haujabadilika,” Bw Gachagua akasema.

Saa chache baadaye, katibu mkuu wa ANC alipuuzilia mbali madai hayo akishikilia kuwa Bw Gachagua hana mamlaka ya kuongea kwa niaba ya muungano huo kuhusu suala hilo.

“Muungano wa Kenya Kwanza haujaamua kuhusu ni nani atakuwa mgombeaji urais na mgombeaji mwenza. Huo ni uamuzi ambao utafanywa na vinara watatu; Dkt William Ruto, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula ‘wakati ufaao’,” akasema Katibu Mkuu wa ANC Simon Gakuru katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Kabla ya Mbw Mudavadi na Wetang’ula kujiunga na UDA na kukabuniwa muungano wa Kenya Kwanza, Bw Gachagua na Mbunge wa Kandara Alice Wahome ndio walikuwa wakipigiwa upatu kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto.

Mnamo Desemba 5, 2021 Dkt Ruto alitoa ishara ya wazi kwamba huenda akamteua Bw Gachagua kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Nataka kuwaomba mruhusu Gachagua kuwa akiandamana nami katika kampeni kote nchini ili tuweze kushinda urais. Mwekeni huru ili aweze kushiriki katika siasa za kitaifa,” Dkt Ruto akawaambia katika eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri, akiwa katika kampeni za kujipigia debe.

Dkt Ruto alimtaja Bw Gachagua kama mwandani wake mwaminifu na kwamba angetaka apige jeki kampeni zake za kitaifa ili aweze kuishinda urais.

Mwanasiasa wengine ambao inadaiwa wanaweza kuteuliwa kuwa mgombeaji mwenza wa Dkt Ruto ni Seneta wa Tharaka Nithi  Kithure Kindiki.

 Profesa Kindiki alijiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana wa kaunti hiyo majuma mawili yaliyopita licha ya uvumi kuenea kuwa angawania kiti hicho.

Seneta huyo alitoa tangazo hilo katika mkutano wa kampeni uliongozwa na Dkt Ruto katika makao makuu ya kaunti ya Tharaka Nithi, mjini Kathwana.

  • Tags

You can share this post!

Kangemi Athletico yazidi RYSA maarifa

Ushauri wa Mzee Moi waacha Kalonzo katika njia panda

T L