Habari

Wetang’ula amwokoa Mutua dhidi ya kiboko cha Mboko

Na LABAAN SHABAAN August 4th, 2024 1 min read

MBUNGE wa Likoni, Mishi Mboko, alianika ‘masaibu ya ndoa’ ya Waziri Mteule wa Leba Alfred Mutua hadharani.

Lakini Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula akakatiza tukio hilo ili kumlinda Dkt Mutua.

Mwanajopo huyo wa Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa alisema ‘skendo za mapenzi’ zinaweza kumharibia sifa Dkt Mutua ambaye alihojiwa kubaini ufaafu wake kuwa waziri.

“Kamati hii haiwezi kuingilia masuala ya ndoa ya mtu yeyote,” Bw Wetang’ula alimkata kalima Bi Mboko aliyeonekana kumuaibisha waziri wa awali wa Utalii na Mashauri ya Kigeni.

“Wakenya wanakutaka upunguze vituko kuhusu maisha yako ya ndoa kwa sababu vinaweza kukuharibia jina ama kukuweka katika hali mbaya,” alisema Bi Mboko.

Mwanakamati mwenza, Omar Abdi Shurie (Mbunge wa Balambala), alionekana ameaibika alipoinama na kuficha uso wake suala hili lilipoibuliwa.

“Mwenyekiti, ni bora utunze masuala yetu ya ndoa yasijulikane na umma,” alisema Bw Shurie kabla ya kukanywa na Spika asiendeleze mjadala huo.

“Hakuna hitaji la mtu kuwa katika ndoa ili atathminiwe kuwa afisa wa umma katika taifa hili,” alisema Bw Wetang’ula.

Habari za utengano kati ya Bi Lilian Nganga na Dkt Mutua mwaka wa 2021 (akiwa Gavana wa Machakos) zilivuma sana na aghalabu suala hili huibuka mara kwa mara.

Baada ya kutengana, Bi Nganga alifunga ndoa na msanii maarufu wa nyimbo za kufoka Julius Owino maarufu Juliani mnamo Februari 2022.