Habari

Wetang'ula angali kiongozi wa Ford-Kenya

June 12th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JOPO la kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa Ijumaa limetamatisha kesi kuhusu mzozo wa uongozi wa chama cha Ford-Kenya huku Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula akisalia kuwa mwenyekiti wake.

Wanachama wa jopo hilo Desma Nungo, Milly Lwanga na Dkt Adelaide Mbithi wameamuru mzozo huo wa uongozi kati ya Seneta Moses Wetang’ula na Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi utatutiliwe na chama hicho.

Punde tu baada ya jopo hilo kutamatisha kesi hiyo, mawakili Ben Millimo, Nelson Havi, Eunice Lumallas na Dkt John Khaminwa wamesema kundi linaloongozwa na Mbunge wa Kimilili Wafula Wamunyinyi litafika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama hicho Jumanne.

“Walioongoza mapinduzi ya kumtimua Bw Wetang’ula katika uongozi wa chama cha Ford-Kenya watafika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama hicho kijibu madai ya utovu wa nidhamu,” amesema Bw Havi aliye pia Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK).

Akiwasilisha ombi la kutamatisha kesi iliyoshtakiwa na Ford-Kenya kupitia kwa Bi Lumallas, wakili mwenye tajriba ya juu Dkt Khaminwa alisema “ pande zote zimekubaliana na zitafute suluhu kulingana na sheria za chama hicho.”

Dkt Khaminwa walijadiliana na wakili Bryan Khaemba, wakili wa Dkt David Eseli Simiyu na Bw Wamunyinyi na wakakubaliana kesi hiyo iondolewe kortini kisha “waisuluhishe kwa mujibu wa Katiba ya chama cha Ford-K.”

Wakili huyo amesema waliwasilisha pendekezo lao kwa afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP) Bi Ann Nderitu ambaye hakulipinga.

“Tumewasiliana na afisi ya RPP kuhusu pendekezo letu na hapingi,” Dkt Khaminwa amesema.

Wakili Wafula Wakoko aliyemwakilisha afisi ya RPP ameliambia jopo hilo hapingi mzozo huo ukirudishwa kwa Ford-K kusuluhishwa kulingana na Katiba yake.

Bi Lumallas na Bw Havi wamefahamisha jopo hilo Bi Nderitu aliandikia chama cha Ford-Kenya barua Juni 10, 2020, akisema chama hicho kiko huru “ kusuluhisha tofauti baina ya viongozi kwa mujibu wa sheria zake.”

Wakitoa uamuzi Bi Nungo, Bi Lwanga na Dkt Mbithi wametamatisha kesi hiyo jinsi ilivyoombwa na Dkt Khaminwa.

“Tunatamatisha kesi iliyoshtakiwa Juni 10, 2020 na kuamuru mzozo huu usuluhishwe kwa mujibu wa sheria na katiba ya chama cha Ford-Kenya,” Bi Nungo aliamuru.

Uongozi wa Ford-K kupitia kwa Bw Wetang’ula ulipinga mapinduzi yaliyoongozwa na baadhi ya maafisa wakuu wa chama hicho.

Kundi linaloongozwa na Bw Wamunyinyi lilichapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali.

Dkt Khaminwa amesema Ijumaa yeye na Bw Khaemba anayewakilisha kundi hilo la Wamunyinyi walikubaliana pia Gazeti hilo linalotambua kundi lake lifutiliwe mbali.

Bi Nderitu ameeleza jopo hilo “Gazeti hilo litasalia tu kwa vile halijaondolewa ama kufutiliwa mbali.”