Habari

Wetang'ula aning’inia padogo kupoteza kabisa Ford-K

June 9th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

SENETA wa Kaunti ya Bungoma Moses Wetang’ula sasa amekaribia kupoteza rasmi uongozi wa chama cha Ford Kenya baada ya msajili wa vyama vya kisiasa kutoa notisi ya kuidhinisha mabadiliko mapya yaliyopendekezwa na Baraza Kuu (NEC) mnamo Mei 31.

Kupitia chapisho kwenye gazeti rasmi la serikali, msajili wa vyama vya kisiasa, Bi Anne Nderitu alitoa notisi ya kuidhinisha kuteuliwa kwa mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi kama kiongozi mpya wa chama hicho.

Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Ford Kenya Chris Mandu Mandu alitemwa na wadhifa huo kupokezwa Bi Josephine Maungu.

“Yeyote ambaye ana malalamishi kuhusu mabadiliko yanayokusudiwa na chama hiki, anahitajika kuandikia afisi ya msajili wa vyama kwa muda wa siku saba baada ya notisi hii,” akasema Bi Nderitu.

Matukio haya yanamzidishia Bw Wetang’ula masaibu, ikikumbukwa aling’olewa kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wengi katika Seneti mwaka wa 2018.

Hii ni licha ya kuwa alishikilia wadhifa huo kwa msingi wa kuwa mmoja wa vinara wa Muungano wa NASA.

Katibu Mkuu Dkt Eseli Simiyu ambaye pia ni mbunge wa Tongaren na Bw Wamunyinyi pamoja na wanachama wengine wa NEC walibadilisha uongozi chamani.

Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati alikuwa kati ya viongozi ambao walihudhuria kikao hicho na kumshutumu Bw Wetang’ula kwa kuongoza chama kiimla, kutoshinikiza umoja chamani na pia kukosa kukivumisha na kukipa sura ya kitaifa.

Hata hivyo, mrengo wa Seneta huyo ulipinga mabadiliko hayo na kumteua Mbunge wa Kiminini Dkt Chris Wamalwa kama Kaimu Katibu Mkuu.

Inasubiriwa kuonekana kama mrengo huo wa Bw Wetang’ula utawasilisha malalamishi kwa msajili wa vyama. Wiki iliyopita, ishara zake kutemwa zilionekana wakati msajili wa vyama alipoambia mrengo wake kwamba, hawakuwa na sahihi za kutosha kufanya mabadiliko waliyodai.

Kwa upande mwingine, mrengo pinzani uliambiwa ukalete sahihi zote za waliohudhuria mkutano wa kumtema seneta huyo katika mamlaka ya chama.

Mapinduzi kwenye chama hicho si jambo geni matukio ya nyuma yakizingatiwa.

Bw Wetang’ula mnamo 2011 alichukua uongozi wa Ford Kenya kwa njia tata kwa kumbandua hasimu wake wa kisiasa Musikari Kombo aliyekuwa kiongozi wa chama wakati huo.

Bw Kombo alichukua usukani mnamo 2004 baada ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais Wamalwa Kijana. Bw Kombo pamoja na Mukhisa Kituyi, Eugene Wamalwa, Raphael Wanjala, Wakoli Bifwoli kati ya wengine walihama na kubuni New Ford Kenya ambacho kilivunjwa kilipojiunga na Jubilee kuelekea uchaguzi wa 2017.

Mnamo 1996 Wamalwa Kijana naye alitokwa jasho baada ya kushiriki mzozo mkali na Raila Odinga waking’ang’ania uongozi kurithi nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha babake Raila, marehemu Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa Kiongozi wa upinzani mnamo 1994.

Ghasia zilizuka wakati wa uchaguzi ulioandaliwa Thika Sports club ulipotibuka huku mirengo ya Bw Odinga na Bw Wamalwa wote wakijitangaza washindi.

Bw Odinga na kundi lake waliondoka na kubuni chama chao cha National Democratic Party (NDP) ambacho alitumia kuwania Urais 1997.