Habari za Kitaifa

Wetang’ula aokoa gari la Salasya lisipigwe mnada

May 18th, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

AGIZO la Spika wa Bunge la Kitaifa Bw Moses Wetang’ula kwa Mahakama ya Madai Madogomadogo, Kakamega, Ijumaa, liliokoa gari linalomilikiwa na Mbunge wa Mumias Mashariki Bw Peter Salasya kupigwa mnada kwa kukosa kulipa Sh500,000.

Bw Wetang’ula aliagiza uamuzi wa awali kubatilishwa, akisema gari hilo linamilikiwa na Bw Salasya na Bunge la Kitaifa kwa pamoja.

Wakili Andrew Emacar, alielezea mahakama kuwa, mbunge huyo alipata mkopo kutoka kwa mwajiri wake kwa kutumia gari hilo kama dhamana.

“Bunge la Kitaifa linamiliki gari hilo, baada ya Bw Salasya kukopa Sh4.2 milioni, ambapo Sh2,789,317 bado hazijalipwa. Bado hajalipa kiasi kamili. Ni kwa manufaa ya haki mfanyabiashara Bw Robert Lutta azuiwe kuendelea na uuzaji wa gari,” alieleza wakili.