Habari Mseto

Wetang’ula aomboleza mwana wa mbunge

January 19th, 2024 1 min read

Na BENSON MATHEKA

SPIKA wa Bunge, Moses Wetang’ula ameomboleza mwana wa Mbunge wa Kibwezi Mashariki Bi Jessica Mbalu, marehemu Benedict Musyoka Mbalu.

Bw Wetang’ula aliungana na familia ya mbunge huyo, viongozi na marafiki kwa ibada ya wafu Alhamisi Januari 18, 2024 katika Kanisa Katoliki la St John the Evangelist, Karen.

“Mawazo yetu yako na familia yako. Tunakuombea nguvu katika wakati huu mgumu wa kuomboleza mwanao mpendwa,” aliongeza.

Huku akimtaja Bi Mbalu kama kiongozi mwenye bidii Bw Wetang’ula alisema kwamba ni huzuni kwa mzazi kupoteza mwanawe.

“Sina maneno ya kutosha kukufariji. Pokea rambirambi zangu na za Bunge kwa kufiwa na mtoto wako mpendwa, Benedict Musyoka Mbalu.”

Spika alisema alifahamu kifo cha Benedict kupitia kwa Karani wa Bunge, Bw Samuel Njoroge, na akahakikishia familia ya mbunge huyo  kwamba Bunge  itasimama nao wakati mgumu wa majonzi.

“Kama mzazi yeyote, hakuna mtu ambaye angependa kumzika mtoto wake, lakini hatuna uwezo wa kuzuia mipango ya Mungu. Tunaamini katika maombi tu na kuishi kwa matumaini kesho kwamba kesho itakuwa bora,” akasema Spika Wetang’ula.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Justin Muturi, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Waziri Soipan Tuya, Wabunge Esther Passaris na Beatrice Elachi na Naibu Katibu wa Bunge la Kitaifa B Serah Kioko ni miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo.