NA BENSON MATHEKA
SPIKA wa Bunge la Taifa Dkt Moses Wetang’ula amesema kwamba kuna haja ya kongamano spesheli la Jumuiya ya Afrika Mashariki la kupiga jeki Bunge la Afrika Mashariki.
Bw Wetang’ula ambaye alizungumza alipokutana na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Mashariki Joseph Ntakirutimana, katika ofisi yake Nairobi alisema shughuli za Bunge la Afrika Mashariki zinapaswa kukuzwa ili liweze kutekeleza majukumu yake.
Spika Ntakirutimana aliandamana na wanachama wa Bunge hilo Hassan Omar, Kanini Kega na Zipporah Kering.
Dkt Wetang’ula alimhimiza Bw Ntakirutimana kutumia tajiriba yake ya miaka mingi kuleta mwamko mpya katika EALA.
Bw Wetang’ula alisema anajivunia katika EALA kwa kuwa alihudumu kama mwenyekiti wa Mawaziri wa nchi za Afrika Mashariki alipokuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kenya ambapo alitekeleza jukumu muhimu jumuiya hiyo kupata wimbo wake wa heshima.
“Hata ukitazama Bunge la Ulaya lilianza kama EALA lakini ndani ya miaka 15 EU ilikuwa imebadilika na watu wote wa nchi wanachama wanaifahamu. Inaweza kufanyika kwa EALA,” alisema.
Alisema kwamba Spika mpya na wabunge wa EALA wako na kazi nyingi ya kufufua na kutia nguvu Bunge hilo lakini ni lazima wapate nia njema ya kisiasa ili kufaulu.
Spika Ntakirutimana alisema kwamba wanalemazwa na bajeti yao ndogo akisema kuna haja ya kuchunguza Ibara 19 ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunda EALA.
Wanachama wengine wa EALA kutoka Kenya ni Falhada Dekow, Kennedy Musyoka, Godffrey Maina, Winnie Odinga, David Sankok, na Shahbal Suleiman.