Wetang’ula kufanya uamuzi mkubwa

Wetang’ula kufanya uamuzi mkubwa

NA CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula Jumatano, Oktoba 5, 2022 anatarajiwa kuamua mvutano kuhusu ni mrengo upi ulio wa wengi katika bunge hilo ili kutoa nafasi ya kubuniwa kwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC).

Jumanne, Bw Wetang’ula alichelea kutoa uamuzi huo na badala yake akatoa nafasi kwa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya kuwasilisha misimamo yao kuhusu suala hilo.

Aliahidi kufanya hivya baada ya wabunge wa pande zote mbili kutoa kauli zao kuhusu mvutano huo.

“Utaratibu ni kwamba shughuli ya kwanza katika kikao cha kwanza mwanzo kwa kila muhula wa bunge huwa ni kuundwa kwa kamati ya kuratibu shughuli za bunge ambayo huongozwa na mimi kama spika. Lakini kwa kuwa kuna utata kuhusu ni upande upi ulio wa wengi na ni upi ulio wa wachache, kamati hiyo haitabuniwa leo,” akasema.

“Vile vile, uamuzi kuhusu suala hilo hautatolewa leo bali nitahiji muda wa kuchunguza masuala yote yanayolizingira kabla ya kutoa uamuzi. Hata hivyo, nitatoa nafasi kwa wote kulizunguzia katika kikao cha leo,” Bw Wetang’ula akaongeza.

Hata hivyo, Spika huyo alithibitisha kupokea orodha ya majina ya wabunge walioteuliwa kuongoza mirengo yote miwili katika bunge hilo, kila upande mmojawapo ukidai wa upande wa walio wengi.

“Kulingana na barua niliyopokea kutoka kwa Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro mnamo Septemba 21, 2022, Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa ameorodheshwa kama kiongozi wa wengi, Naibu wake ni Mbunge wa Kilifi Owen Baya. Naye Bw Osoro mwenyewe anajirejelea kama kiranja wa wengi huku naibu wake akiwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Marsabit Naomi Wako,” Bw Wetang’ula akasema.

“Kutoka mrengo wa Azimio nilipokuwa barua kutoka kwa Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed iliyoorodhesha Opiyo Wandayi kama kiongozi wa wengi huku naibu wake akiwa Mbunge wa Kathiani Robert Mbui. Alijitaja kama kiranja wa wengi huku naibu wake akiwa Mbunge Maalum Sabina Chege,” akaongeza.

Wakati wa mjadala kuhusu suala hilo Bw Ichung’wa alidai kuwa Azimio sio muungano wa vyama na kwamba ni chama cha muungano na hivyo haitambuliwi bungeni kwa mujibu wa kipengele cha 108 cha Katiba.

“Kulingana na kipengele hiki cha katiba mrengo wa walio wengi bungeni ni chama cha kisiasa au muungano wa vyama wenye idadi kubwa bungeni. Kwa misingi hii Kenya Kwanza ndio muungano wa vyama ulio na idadi kubwa ya wabunge,” akaeleza Mbunge huyo wa Kikuyu.

Bw Ichung’wa alishikilia kuwa ni mgombea urais Bw Raila Odinga pekee ambaye ndiye mwanachama wa Azimio kama chama cha kisiasa.

Aidha, Mbunge huyo aliongeza kuwa wabunge wa vyama vilivyotangaza kuhama Azimio walikuwa na haki yao kikatiba kuchukua uamuzi huo kwa msingi wa kipengele cha 38 cha Katiba kuhusu haki ya kufanya maamuzi ya kisiasa.

Lakini Bw Wandayi ambaye ni Mbunge wa Ugunja alishikilia kuwa kwa mujibu wa sharia za vyama vya kisiasa ya 2022, Azimio inachukuliwa kuwa chama cha muungano na muungano wa vyama vya kisiasa.

“Azimio ina jumla ya vyama tangu 26 na muungano wa vyama. Kufikia sasa hakuna chama hata kimoja miongoni mwa vyama hivyo kimefaulu kujioondoa rasmi,” akasema.

Bw Wandayi alishikilia kuwa, kisheria Azimio ina jumla ya wabunge 173 ilhali Kenya Kwanza ina wabunge 164.

Lakini Bw Ichung’wa alishikilia kuwa baada ya Kenya Kwanza kuwanasa wabunge kadha wa vyama vya United Democratic Movement (UDM), Kanu, Pamoja African Alliance (PAA) na Maendeleo Chap Chap na Movement for Growth and Development (MDG) idadi ya wabunge wa mrengo huo imetimu 183.

  • Tags

You can share this post!

Bobi Wine na Besigye washutumu Jenerali Muhoozi Kainerugaba

Liverpool wacharaza Rangers 2-0 katika gozi la UEFA ugani...

T L