Habari Mseto

Wezi wa kuku waua familia nzima ya watu wanne

February 21st, 2020 1 min read

Na DERICK LUVEGA

MFANYABIASHARA kutoka Vihiga, mkewe na watoto wake wawilli waliuawa kwa kukatwakatwa mnamo Ijumaa asubuhi na genge la vijana saba waliotaka kuiba kuku kutoka kwa boma lao Busamu, na kuongeza orodha ya visa vya uhalifu vinavyokumba eneo hilo.

Wahanga hao: Bw Kennedy Ambani anayemiliki duka la kuuzia dawa za mifugo katika kituo cha kibiashara cha Magada, mkewe Elizabeth Achieng’, Gifton Ambani (mwana wao) na binti yao Ann Ambani walikuwa na majeraha kadha ya panga kwenye miili yao.

Mwanamume huyo, mkewe na mtoto wao wa kiume walifariki papo hapo wakati wa tukio hilo la saa nane usiku wa manane.

Mtoto wao wa kike alifariki kutokana na majeraha katika Hospitali Kuu ya Kakamega ambapo alikuwa amelazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU).

Kisa hicho kimejiri kufuatia kisa sawa na hicho mnamo Jumatatu ambapo genge lilimuua mwanamume na mkewe katika kijiji jirani cha Ingidi, ambapo mbuzi wanne na kuku waliibwa.

Kamanda wa Kaunti Hassan Barua alithibitisha tukio hilo akisema majina ya washukiwa yamekabidhiwa polisi na uchunguzi umeanzishwa.

Umati wenye ghadhabu ulimuua kwa kumteketeza mshukiwa mmoja aliyeaminiwa kuwa sehemu ya genge hilo lililoshambulia familia hiyo.

Boma hilo liko kando ya Kituo cha Polisi cha Magada lakini ni maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Mbale waliokuwa wa kwanza kuwasili hapo.

“Tulielezwa kwamba genge la vijana saba lilivunja nyumba ya wahasiriwa na kuwaua kwa kuwakatakata. Walinuia kuiba kuku,” alisema Bw Barua.