Habari Mseto

Wezi wa ng'ombe wakimbilia usalama kituo cha polisi

June 7th, 2020 1 min read

NA CHARLES WANYORO

Kulishuhudiwa kizaazaa katika kituo cha polisi cha Nkubu Kaunti ya Meru baada ya wezi wawili wa ng’ombe kujisalimisha huku wakihepa umati wa watu uliokuwa na ghadhabu tayari kuwakabili Jumamosi usiku.

Wawili hao, mwanamke na mwanaume walikimbizwa na wakazi wa Kieni Kia Ndege kabla ya kutafuta maficho kwa kituo cha polisi saa saba unusu usiku.

Wenzao watatu wanaoaminika kuwa sehemu ya genge la wizi wa mifugo Kaunti ya Meru walihepa kwa mguu niponye.

Akisimulia kisa hicho, mwanabiashara mmoja Bw Murithi Senior alisema kwamba gari ndogo lenye usajili wa KBA673H lilionekana likisafirisha ng’ombe wawili.

“Niliwaita vijana na watu waliokuwa wameibiwa ng’ombe hapo awali na tukangoja karibu na barabara. Tuliwakimbiza wakaangusha ng’ombe mmoja katikati ya barabra ili kutupumbaza na wakageukia njia ya mchanga baadaye waliachilia tairi na bado tukaendelea kuwafuata huku tukipiga kelele,” alisema

“Huku tukiendelea kuwakimbiza magari mengine 12 yalijunga nasi na washukiwa hao kwa haraka wakakimbililia kwa kituo cha polisi.”

Diwani wa eneo hilo John Paul Kireria alisema kwamba wamepoteza ng’ombe 30.