Habari Mseto

Wezi waiba mali ya maelfu katika kanisa

October 15th, 2019 1 min read

Na STEVE NJUGUNA

WAKAZI mjini Nyahururu, Kaunti ya Laikipia wameshangazwa na jinsi watu wasiojulikana walivyovamia kanisa na kulipora mali ya thamani kubwa.

Wezi waliingia katika Kanisa Anglikana (ACK) la Nyahururu kupitia dirisha walilovunja.

Kulingana na Askofu Stephen Kabora anayesimamia dayosisi ya ACK Nyahururu, wezi hao walifika hadi katika chumba cha kuhifadhi mali za thamani za kanisa na wakaiba vitu tofauti pamoja na kiasi kisichojulikana cha pesa.

Bw Kabora alisema wezi hao waliiba pia kinanda, chombo cha kuunganisha mitambo ya muziki na televisheni mbili ambazo zote ni za thamani ya Sh255,000.

“Tulishtuka tulipoingia katika uwanja wa kanisa tukaona dirisha moja likiwa limevunjwa. Tulipoingia ndani tulipata vifaa kadhaa vya elektroniki vilikuwa vimeibiwa,” akasema.

Askofu huyo alikashifu kisa hicho na kusema ni ukosefu wa heshima kwa jumba la kusali.