Wezi wakata vyuma vya daraja la Makupa

Wezi wakata vyuma vya daraja la Makupa

WACHIRA MWANGI na SIAGO CECE

WASIWASI umetanda miongoni mwa wakazi wa mji wa Mombasa wakiwa na hofu kuwa daraja la Makupa litabomoka.

Hii baada ya wezi kuvamia daraja la Makupa na kuiba vyuma vinavyoshikilia daraja hilo.

Wezi hao walikata vyuma chini ya daraja la Makupa lenye urefu wa mita 120 linalouganisha kisiwa cha Mombasa na Changamwe.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo uligundua kuwa zaidi ya mita 20 ya vyuma katika upande moja wa daraja hilo vimekatwa. Ripoti pia zinasema upande mwingine wa daraja hilo pia limevamiwa na vyuma kung’olewa.

Tayari, kuna vyuma vimening’inia chini ya daraja hilo linalotumiwa na matrela nzito zinazosafirisha mizigo kutoka Bandarini.

Daraja la Makupa lilijengwa karne moja iliyopita na wakoloni na ndio barabara kuu ya kuingia na kutoka kisiwa cha Mombasa.

Madereva na wakazi wanaotumia daraja hilo hata hivyo wamekuwa na hofu kuhusu kuporomoka kwake.

Kulingana na shahidi mmoja, alisema wezi wao walikuwa na vifaa vinavyotumia gasi kukata vyuma hivyo mwezi moja uliopita.

“Walikuwa hapa mwezi jana. Nilipojaribu kuwakataza walinifunga na kunipiga na kuendelea na wizi. Niliripoti kwa polisi,” ashahidi huyo ambaye hakutaka kutajwa alieleza.

Kulingana na wataalamu, jambo hili lisipotatuliwa mapema litasababisha daraja hilo kuporomoka.

Mhandisi wa ujenzi Stanley Bett, alisema uharibifu huo utafanya daraja likose msingi mzuri na linaweza kuanguka wakati wowote.

“Kwanza, daraja litakuwa na nyufa. Baadaye ikiwa halitarekebishwa, linaweza kuporomoka,” alieleza Bw Bett.

Hata hivyo Mamlaka ya Barabara Kuu Kenya (KeNHA) imewatuliza wakazi ikisema tayari marekebisho yameanza kwenye daraja hilo lililojengwa juu ya bahari.

“Kuna kikundi ambacho kimeenda kukagua hali ilivyo. Tayari vyuma vinne vimeibwa lakini hakuna madhara kuu iliyofanyika ambayo ni hatari kwa watumizi wa barabara,” alieleza Bw Charles Njogu, afisa mkuu wa mawasiliano KeNHA.

Alisema pia KeNHA imeimarisha usalama katika daraja hilo katika ili kuzuia uharibifu zaidi wa muundo huo.

“Waendeshaji magari wanahimizwa kuwa wavumilivu kwani hatua za kurekebisha zinaendelea,” ilisema Bw Njogu.

Washukiwa sita wa uvamizi tayari wamekamatwa katika zoezi lililofanywa Jumanne usiku karibu na barabara kuu ya Makupa mjini Mombasa.

Operesheni ya mashirika mengi iliyoongozwa na afisa wa uchunguzi wa Changamwe, Polisi na wazee wa Nyumba Kumi walivamia makazi ya Hodi B ambapo walipata tani kadhaa za vyuma na waya za stima na vifaa kadhaa vya umeme.

Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi Chaani wakisubiri kufikishwa mahakamani.

KeNHA amewataka wakazi macho na kuripoti visa vyovyote vya uhalifu vinavyoendelea katika barabara hiyo.

You can share this post!

Europa: Man-Utd vs Granada, Arsenal vs Slavia Prague

MAUYA OMAUYA: Shujaa Magufuli: Hakika chema kamwe hakidumu