NA MACHARIA MWANGI
AINA mpya ya uhalifu imechipuka katika barabara za Naivasha ambapo kundi la walaghai wanazunguza wakijifanya kuangusha bunda la noti kisha wanawaibia wakazi.
Kulingana na ripoti ya kituo cha polisi cha Naivasha, watu wanne wameibiwa na walaghai hao, mmoja wao akipoteza zaidi ya Sh300,000 juzi.
Kulingana na makachero, wezi hao kwanza hutambua mtu wanayepania kumwibia, kisha wakafuatilia mienendo yake, kabla ya kutekeleza kibarua chao.
“Wao hutembea kwa makundi ya watu wawili au watatu. Mmoja wao kurusha bunda la noti mbele ya anayelengwa. Mtu huyo akiingia mtegoni kwa kujaribu kuokota noti hizo, hapo ndipo wezi hao humvamia na kumwibia,” akasema mmoja wa wapelelezi.
Wengi ambao wamewahi kuibiwa walikubali kuwa walijaribu kuokota pesa hizo lakini dakika chache wanachama wa genge hilo hutokea na kudai kuwa wao pia waliona pesa hizo “zilizoangushwa na mwenye bila kufahamu.”
“Walaghai hao huahidi kugawana pesa hizo kwa usawa na mtu wanayepanga kumwibia. Kisha wao humvuta katika eneo fiche ambapo aliyeangusha pesa hutokea na kudai anataka arejeshewe pesa zake zote,” akasema afisa huyo.
“Ni wakati huo ambapo walaghai hao hutaka kuona masalio ya pesa kwenye akaunti yake ya Mpesa kutoka kwa jamaa wanayelenga kumwibia. Wezi hao hufuatilia kwa makini anapobonyeza nambari yake ya siri (PIN) kwa woga na hivyo ndivyo wao hujua nambari ya mtu huyo kwa urahisi,” afisa huyo anaongeza.
Baada ya hapo, walaghai hao hutwaa simu ya mtu huyo na kutoa pesa zote kwenye akaunti yake ya Mpesa kisha wakatoweka na kumwacha hoi.
Wahudumu wawili wa afya ni miongoni mwa watu ambao wamewahi kuibiwa na walaghai hao ambao sasa wanasakwa na polisi.
Isaac Kangatu, alielezea namna alivyovutiwa na walaghai hao mnamo Februari 6, 2023 alipokuwa akitembea katika barabara za mji wa Naivasha.
“Ilikuwa ni mwendo wa saa kumi za jioni pale mwanamume wa umri wa makamo aliokota kitu kando yangu. Alinionyesha bunda la noti za Sh1000 zilizofungwa kwa kamba ya mipira,” akasema.
“Sikuwa na haja lakini akanishawishi kwamba kwa sababu nilimwona akiokota pesa hizo, ilikuwa jambo la busara kwamba tugawane pesa hizo,” Bw Kangatu akaendelea kusema.
Ni baada ya hapo ambapo aliibiwa jumla ya Sh20,600 ambazo zilikuwa katika akaunti yake ya Mpesa.