Habari za Kaunti

Wezi wapika chamcha kwa nyumba za walioenda kazini

January 5th, 2024 1 min read

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa Karagita viungani mwa mji wa Naivasha katika Kaunti ya Nakuru wameripoti ongezeko la visa vya wezi ambao,  huwa hawana haraka ya kuenda zao kwani wanapika chakula cha mchana kisha wanaondoka na bidhaa wanazokuwa wameiba.

Walalamishi hao pia wamewakosoa machifu na wazee wa Nyumba Kumi kwa kushindwa kudhibiti wezi hao ambao hurukia uani na kuingia kwenye makazi ya kibinafsi, mchana peupe wenyeji wakiwa kazini.

Bi Sarah Nduta, mkazi wa South Lake, anasema kwa kawaida wahalifu hulenga maboma ya wakulima wadogo, wanaofanya shughuli za ufugaji wa ng’ombe au kuku.

Taifa Leo imeambiwa na walalamishi kwamba wahusika huwa wamejipanga kwelikweli.

Huanza kwa kuvunja milango na kuingia chumbani kisha wakapumzika na hatimaye kupika kabla ya kuondoka na vyombo vya thamani kubwa.

Katika eneo la Karagita baadhi ya wakazi wametaja ongezeko la visa vya uhalifu kwa sababu ya kupungua kwa samaki katika Ziwa Naivasha.

Hii ikitokana na kile kinachodaiwa kwamba vijana wengi hawana kazi.

Bi Ruth Mokaya ambaye ni muuzaji wa samaki katika eneo hilo, anasema wezi wamekuwa wakivunja nyumba za watu nyakati za mchana wakati ambapo wenye nyumba huwa wako kazini.

Anasema yeye pia ni mfugaji wa kuku na mbuzi ila wiki hii alishangaa alipotoka kazini na kupata kibanda chake cha kuwafugia kuku kimevunjwa.

Na kama haitoshi, jikoni walikuwa wamepika sima na mifupa ya kuku ilikuwa imetapakaa kuanzia mlangoni hadi sebuleni.

Kulingana na Bi Mokaya, hii sio mara ya kwanza kupitia changamoto kama hii.  Anasema ingawa aliripoti kisa chenyewe kwenye kituo cha polisi, washukiwa hawajulikani.