Habari Mseto

Wezi wavunja kanisa na kuiba mahindi

September 17th, 2018 1 min read

MAGATI OBEBO na SHABAN MAKOKHA

WEZI ambao idadi yao haijabainishwa, mnamo Jumamosi, walivunja na kuingia kanisa la Ekerubo Seventh Day Adventist, Masaba Kusini, Kaunti ya Kisii na kuiba vifaa vya muziki na gunia la mahindi.

Mzee mmoja wa kanisa hilo, Bw Jairus Ombogo, aliambia Taifa Leo kwamba washiriki walishangaa kupata habari za kisa hicho Jumapili asubuhi.

Alisema walikuwa wakikadiria hasara kabla ya kupiga ripoti kwa maafisa wa usalama wafanye uchunguzi.

“Tulimfahamisha pasta wa kanisa kulingana na utaratibu kabla ya kisa hiki kuripotiwa rasmi kwa polisi,” alisema Bw Ombogo.

Kwingineko, polisi katika Kaunti ya Kakamega wanamzuilia mwanamume aliyemshambulia na kumuua jirani yake kufuatia mzozo wa ardhi.

Inadaiwa Bw Fredrick Mangala, mkazi wa kijiji cha Irobo, kata ya Museno, Kakamega alimshambulia na kumuua Bw Fredrick Machanga kufuatia ugomvi wa miaka mingi wa kipande cha ardhi.

Mkuu wa upelelezi wa eneo la Shinyalu (DCIO), Bw Paul Gathara alisema marehemu alipigwa risasi upande wa kulia wa kifua na kufariki papo hapo.

“Suala hilo liko kortini. Kesi itasikizwa Septemba 25 lakini wawili hao walianza kupigana na mmoja akauawa,” alisema Bw Gathara.

Bw Mangala alijisalimisha kwa polisi baada ya kumuua jirani yake.

Gathara alisema polisi walitembelea eneo la mauaji na kupata maganda ya risasi iliyotumika kumuua Machanga.

“Pia tumechukua bastola ya mshukiwa alipojiwasilisha kwa polisi,” alisema Bw Gathara.

Wakazi walisema ardhi inayobishaniwa ni ya marehemu ambayo alirithi kutoka kwa marehemu baba yake na aliyemuua alitaka kumpokonya.