Kimataifa

WHO yahimiza Wake wa Marais Afrika wayakabili maradhi hatari sana

December 4th, 2019 2 min read

Na AFP

KIONGOZI wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus, mnamo Jumatatu aliwahimiza Wake wa Marais barani Afrika kuwezesha ‘nia ya kisiasa’ katika kuangamiza ueneaji wa Ukimwi hasa miongoni mwa watoto.

Akizungumza katika kongamano la kimataifa kuhusu ukimwi jijini Kigali, Rwanda, Ghebreyesus alisema Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU), homa ya ini na kaswende ni maradhi hatari sana Afrika.

Alisema maradhi yote hayo matatu yanayoweza kupitishwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto, ni hatari na huwa mzigo mkubwa kwa mifumo ya afya. Aidha, alisema maradhi hayo huwa yenye gharama kubwa kwa familia hivyo kufanya wanajamii kuwa fukara, ilhali magonjwa hayo yote matatu yanaweza kuzuiwa.

“Kukomesha usambazaji wa mama kwa mtoto kuhusu HIV, kaswende na homa ya ini kunawezekana na nyinyi (kina mama taifa) mnaweza kusaidia kutoa kiungo muhimu kuyakabili,” Ghebreyesus alieleza hadhira iliyojumuisha wake wa marais kutoka Rwanda, Congo Brazzaville, Chad, Niger, Ghana na Botswana.

Maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika yanaongoza katika kukomesha usambazaji wa HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto, huku jumla ya asilimia 92 ya kina mama wajawazito wakipokea matibabu ya kuzuia makali ya virusi hivyo kwa mujibu wa WHO.

Mama Taifa Rwanda, Jeannette Kagame alitoa wito kuwepo kwa majadiliano wazi kuhusu dhuluma za kijinsia, suala alilosema linalemaza juhudi za kuangamiza ukimwi.

Akifungua kongamano hilo, Rais wa Rwanda Paul Kagame alieleza kuwa katika maambukizi ya zinaa, unyanyapaa na kukaa kimya ndicho kiini kikuu cha vifo kando na virusi kwa kuwa huwazuia watu dhidi ya kujifunza kuhusu magonjwa hayo na kukubali hali zao.

Huku akisema kwamba ukimwi haufahamu mipaka, Kagame alitoa wito kwa serikali Afrika kuongeza kiasi cha fedha katika bajeti kinachotengewa sekta ya afya. Mnamo 2018, watu 770,000 walifariki kutokana na HIV huku watu 1.7 milioni wakiambukizwa upya, ambapo idadi kubwa ya visa hivyo na vifo vilitokea Afrika kulingana na WHO.

Kwa mujibu wa WHO, watu zaidi ya 37 milioni walikuwa wakiishi na HIV kote ulimwenguni mnamo 2018, huku Afrika kukiwa na angalau mtu mmoja miongoni mwa kila watu 25 walioambukizwa virusi hivyo.