Kimataifa

WHO yakemea nchi kuhusu mbinu duni kukabili Corona

March 7th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) limeonya kuwa nchi nyingi ulimwenguni hazijachukua hatua madhubuti za kukabiliana wala kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona na kusisitiza kuwa maradhi hayo hatari hayafai kuchukuliwa kimzaha.

Hayo yalijiri huku maradhi hayo yakiathiri uchumi, michezo na shughuli za kidini ulimwenguni.

WHO lilisema hayo huku maradhi hayo yakienea kwa kasi barani Ulaya na Amerika ambako matabibu wanalalamikia hatua ya hospitali kukosa kujiandaa kuyakabili.

Biashara iliathiriwa kote ulimwenguni na kuzidisha wasiwasi kuhusu hali ya uchumi mataifa yakishughulika kukabili maradhi ambayo kufikia jana yalikuwa yameua watu 3,500 na zaidi ya 100,000 kuambukizwa katika mataifa 90.

Idadi ya watu walioambukizwa iliongezeka katika mataifa ya Italia, Ufaransa, Ugiriki na Iran huku meli ya kifahari ikizuiwa katika ufuo wa California, Amerika ili abiria waliokuwa na dalili za homa hiyo wapimwe ilivyofanyika Japan wiki chache zilizopita.

Maradhi hayo yameathiri vibaya biashara, utalii, michezo na masomo huku wanafunzi 300 milioni kote ulimwenguni wakitakiwa kukaa nyumbani.

Hata shughuli za kidini zimeathiriwa na kuenea kwa maradhi hayo. Makao makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican yalitangaza kuwa, Papa Francis huenda akabadilisha ratiba yake, mji wa Bethlehem ulitengwa na Saudi Arabia ikafunga eneo takatifu la Waislamu jijini Mecca.

China ambako virusi hivyo vilianzia mwaka 2019 inaendelea kushuhudia vifo vingi na maambukizi mapya yakiongezeka kwa kasi katika mataifa kama Korea Kusini, Iran na Italia.

Mnamo Alhamisi, WHO ilionya kuwa mataifa mengi hayakuwa yameonyesha nia halisi ya kisiasa ya kukabiliana na tisho inayokodolea macho kila mtu.

“Hili sio zoezi,” Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliambia wanahabari.

Akaoneza: “Mkurupuko huu ni tisho kwa kila nchi, maskini na tajiri.”

Tedros alihimiza viongozi wa serikali katika kila nchi kusimamia na kushirikisha sekta zote kujiandaa kukabili maradhi haya badala ya kuachia mawaziri wa afya.

“Kinachohitajika ni maandalizi makali, alisema. Nchini Amerika, utafiti wa chama kikubwa cha wauguzi ulionyesha hali ya kusikitisha ya maambukizi. Matokeo yalionyesha kuwa asilimia kubwa ya hospitali za nchi hazijajianda kushughulikia maradhi haya,” alisema Jane Thomason, mtaalamu wa chama hicho.

Visa vipya vya maambukizi viliripotiwa China ambako miji ilisalia mahame baada ya mamilioni ya watu kufungiwa kufuatia kuenea kwa maradhi hayo.