Habari Mseto

WHO yaomba nchi kuchangia kampeni ya kudhibiti Malaria

December 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MAMIA ya watu bado huambukizwa malaria kila mwaka huku ugonjwa huo ukiua zaidi ya watu 400,000 –wengi wao wakiwa watoto barani Afrika- kwa sababu juhudi za kupambana na maradhi hayo zimekwama, Shirika la Afrika Ulimwengu (WHO) limesema.

Inakadiriwa kuwa mtoto mmoja hufariki kutokana na malaria kila baada ya dakika mbili.Shirika hilo lilisema ufadhili wa vita dhidi ya ugonjwa huo umesitishwa, hali inayowaacha nusu ya watu duniani katika hatari ya kuambukizwa malaria unasambazwa na mbu.

WHO sasa inatoa wito mataifa wafadhili na serikali za nchi ambazo zimeathirika na ugonjwa huo kuimarisha mikakati ya kupambana nao kwa kuongeza ufadhili wa mipango ya kupambana na malaria.

“Ulimwengu umeonyesha kuwa hatua inaweza kufikiwa katika vita dhidi ya ugonjwa huu,” mtaalamu wa malaria katika WHO, Pedro Alonso aliwaambia wanahabari jana.

Alitoa mfano wa kupungua kwa visa vya maambukizi na vifo tangu 2010 wakati visa hivyo vilipungua kutoka 239 milioni hadi 214 milioni duniani mnamo 2015.

Na vifo kutokana na malaria vilipungua kutoka watu 607,000 hadi takriban watu 500,000 mnamo 2013.

“Lakini mafanikio hayo yamepungua kwani viwango vya maambukizi bado ni juu,” Alonso akasema.

Mnamo 2018, visa vya maambukizi ya malaria vilipungua kwa kiwango kidogo – hadi 228 milioni kutoka watu 231 milioni mnamo 2017.

Na idadi ya vifo ilipungua hadi watu 405, 000 kutoka 416,000 mnamo 2017 ulimwenguni.

Kati ya vifo vilivyorekodiwa mnamo 2018, takriban 380,000 vilitokea barani Afrika; asilimia 25 ya vifo hivyo vikiripotiwa kutoka nchini Nigeria pekee.

Kulingana na ripoti ya WHO, wanawake wajawazito na watoto barani Afrika waliendelea kuathirika zaidi na malari mwaka jana.

Takribani wanawake 11 milioni waja wazito katika mataifa yaliyoko chini ya Jangwa la Sahara waliathirika na malaria mnamo 2018.

Hali hiyo ilisababisha takriban watoto 900,000 kuzaliwa wakiwa na uzani wa chini, na hivyo maisha yao kuwa hatarini.

Ripoti hiyo ya WHO pia imebaini kuwa, mnamo 2018, zaidi ya thuluthi moja ya watoto katika mataifa ya Afrika yaliyoko chini ya jangwa la Sahara hawakuwa wakilala chini ya neti za mbu za kuwakinga dhidi ya maambukizi.

Mnamo Novemba, jarida la ‘Science Magazine’ liliripoti kwamba chanjo ya kwanza dhidi ya malari ilizinduliwa katika mataifa ya Ghana, Malawi na Kenya.

Wakati huo huo, iliripotiwa Novemba kwamba mwanajeshi wa China anayehudumu katika kikosi cha kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa (UN) alifariki kutokana na malari akiwa kazini nchini Sudan Kusini.