WHO yatoa tahadhari ya corona kuleta kisonono sugu

WHO yatoa tahadhari ya corona kuleta kisonono sugu

Na LILIAN NDILWA

MADAKTARI kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni wameonya kuhusu maambukizi mapya ya ‘kisonono sugu’ kinachoaminika kusababishwa na virusi vya corona.

Ugonjwa huo wa zinaa umekuwepo kwa muda mrefu, lakini kulingana na madaktari, maambukizi haya ni aina ya kisonono sugu kinachokataa kabisa kusikia dawa na matibabu yaliyopendekezwa dhidi yake.

Maambukizi sugu ya kisonono tayari yalikuwa yameripotiwa na mataifa kadhaa ikiwemo Ufaransa, Japan, Uhispania, Uingereza na Australia.

Kulingana na Afisa wa Matibabu katika Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt Teodora Wi, sababu za kuongezeka kwa maambukizi ya kisonono sugu ni matumizi ya aina mbalimbali ya dawa kali kukabiliana na virusi vya corona.

Alitaja dawa za kuangamiza maradhi yanayosababishwa na bakteria kuwa miongoni mwa hizo, kando na matumizi kupita kiasi ya dawa husika, yote ambayo ni masuala yanayohusiana na COVID-19.

Dkt Wi alifafanua katika ripoti ya WHO kuwa hali ya kukataa kusikia dawa dhidi ya bakteria katika kisonono iliibuka muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa matumizi ya dawa hizo mwanzoni mwa karne ya 20, ambapo hali hiyo imezidi kuendelea tangu wakati huo.

“Kuna uwezekano kwamba hali hiyo ya kukataa kusikia dawa huenda ikaonekana katika maambukizi mengineyo ya zinaa. Kwa hakika, tayari tumeanza kushuhudia hali hiyo kwa sababu kuna ongezeko la Mycoplasma genitalium, ambayo ni aina maarufu ya ugonjwa wa zinaa unaosababisha mfereji wa mkojo kutoa uchafu,” alisema Dkt Wi.

Alisema kutakuwa na matatizo mengi endapo kisonono hakitatibiwa ipasavyo au ikiwa ugonjwa huo utageuka kuwa usioweza kutibika kwa kutumia dawa za kawaida za kuangamiza bakteria.

“Kuna athari nyingi za kuibua wasiwasi, kwanza ni matatizo ya uzazi ambapo kutakuwa na ongezeko la maambukizi ya HIV, kukosa nguvu za uzazi na maambukizi sugu ya macho ambayo huenda yakasababisha upofu,” inasema ripoti hiyo ya WHO.

Alitaja athari nyingine kama vile kusambaa kwa maradhi kufuatia aina mbalimbali za zinaa zisizosikia dawa. WHO inaeleza wazi kwamba ugonjwa huo wa zinaa huenda ukawa hata sugu zaidi dhidi ya matibabu yaliyopendekezwa kama vile azithromycin, ambazo ni dawa zinazotumiwa kutibu maambukizi ya kifua na mishipa ya pua.

Kumekuwa na ongezeko la matumizi ya Azithromycin wakati wa janga la Covid-19.

You can share this post!

MARY WANGARI: Tuwe na matumaini 2021 itakuwa yenye heri...

Hakuna wa kunizuia kuwania ugavana Nairobi – Baba Yao