Habari za Kitaifa

Uchunguzi: Wi-Fi ya bure haifanyi kazi katika kaunti nyingi Kenya

April 27th, 2024 1 min read

NA WAANDISHI WETU

UCHUNGUZI wa Taifa Leo umebaini kuwa mawimbi ya mawasiliano ya intaneti ya Wi-Fi ya bure iliyozinduliwa katika vituo mbalimbali nchini na serikali ya Kenya Kwanza hayafanyi kazi.

Katika baadhi ya maeneo kama vile Kaunti za Kisumu, Siaya, Kwale, Mombasa, Laikipia na Turkana, mifumo ya Wi-Fi, ama iliacha kufanya kazi miezi michache baada ya kuzinduliwa au ikiwa inafanya kazi, basi intaneti hiyo haiko thabiti.

Katika Kaunti ya Kwale, wafanyabiashara katika soko la Diani wanalalamika kuwa hawajafaidika na mpango huo.

“Tulikuwa na imani kuwa mpango huo ungeimarisha biashara zetu ila hatujaona faida yake. Wi-Fi ya bure iliacha kufanya kazi Oktoba 2023,” akasema Sebastian Juma, mfanyabiashara katika soko hilo.

Katika Kaunti ya Mombasa, mpango huo uliacha kufanya kazi miezi sita iliyopita.

Kwa upande mwingine, wafanyabishara katika Kaunti ya Nairobi, Turkana na Trans Nzoia pia wametoa malalamishi yao kuhusu mpango huo wa serikali wakisema hawajanufaika na mradi huo.

Hata hivyo, wafanyabiashara kutoka Kaunti za Siaya na Nandi waliusifu mpango huo wakisema unafanya kazi ipasavyo.

Mei 2023, Rais William Ruto aliahidi kuwa serikali yake itaweka mawimbi ya mawasiliano ya WI-FI ya bure katika jumla ya vituo 25,000 kote nchini.

Kulingana na Dkt Ruto, mpango huo ulilenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kuendeleza biashara za mitandaoni kupitia mfumo ujulikanao kwa kimombo kama, ‘e-commerce’.

“Wale ambao watanufaika zaidi katika mpango huu wa mtandao wa mawasiliano bila kulipiwa ni mamilioni ya vijana hawa wetu ambao huendesha shughuli nyingi mitandaoni,” Rais alisema.

Mnamo Aprili 2023, Benki ya Dunia ilitangaza kuwa imetoa Sh52 bilioni kufadhili mpango huo.

Uzinduzi wa Wi-Fi ya bure ulikuwa ukifanywa na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Uchumi Dijitali Eliud Owalo.