Wiki ya ubunifu yaanza rasmi

Wiki ya ubunifu yaanza rasmi

Na WANGU KANURI

WIKI ya Ubunifu iling’oa nanga kwa mara ya kwanza nchini, katika shule ya serikali iliyoko katika eneo la Lower Kabete, Nairobi, huku Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha akisisitiza kuwa ni muhimu kwa ubunifu kukua ili uchumi uweze kuendelea.

Akipigia debe Shirika la Ubunifu nchini (KeNIA) kwa kuanzisha wiki hiyo ya ubunifu, Profesa Magoha alieleza kuwa ishara ya ukuzi wa kitaifa ni mifumo imara ya ubunifu. Baada ya janga la corona kuvamia nchi ya Kenya, uchumi ulidorora sana kwani watu wengi walipigwa kalamu.

Akifungua rasmi ukumbi huo, Waziri wa Habari na Teknolojia Bw Joseph Mucheru alieleza kuwa nyakati za Covid-19 zilitarajiwa kuleta nafasi katika nyanja za Utafiti, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu. Nafasi hizo zilipaswa kuhakikisha kuwa uchumi umeendelea fauka ya changamoto zilizoletwa na ugonjwa huo.

“Ulimwenguni kote, uchumi hukua na kuendelea iwapo ubunifu wa wananchi utazingatiwa na kutumiwa kikamilifu. Vile vile, kuwepo kwa mazingira mazuri yatakayorahisisha huduma na bidhaa kufika soko mbalimbali kunasaidia uchumi kukua,” akaeleza.

Dhima kuu ya wiki hiyo ni ‘Ubunifu wa Wakenya,’ huku ushirikiano wa washikadau kutoka sekta za kibinafsi, umma na kimataifa ukitarajiwa kuundwa.

Hali kadhalika, Waziri Mucheru alisisitiza kuwa kubuniwa kwa utamaduni wa utafiti, maendeleo na ubunifu nchini Kenya kunalenga kuboresha utengenezaji bidhaa, kupunguza gharama, kuimarisha ushindani baina ya washikadau na kuboresha manufaa.

Wiki hiyo ya Ubunifu inatarajiwa kuendelea kutoka Desemba 6 hadi Desemba 10 mwaka huu. Vile vile, miradi ya nchi chini ya Ajenda Nne Kuu na Ruwaza ya 2030 inanuiwa kuendelezwa kwenye wiki hiyo ya ubunifu.

“Ruwaza ya 2030 imelenga kuhakikisha kuwa taifa la Kenya limeendelea ndiposa tunapaswa kuimarisha taasisi zetu za kujifunza kwa ujuzi unaohitajika hivi sasa kwenye soko,” Waziri Mucheru akaongeza.

You can share this post!

Mwendwa atupwa seli tena baada ya kukana mashtaka

WANYONYI SUPER CUP: Kivumbi kikali mechi za Tim Wanyonyi...

T L