Wilbaro ya Ruto imeshika kutu, Kieleweke wadai

Wilbaro ya Ruto imeshika kutu, Kieleweke wadai

Na MWANGI MUIRURI

WANASIASA wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta wamewakejeli wenzao walio upande wa Naibu Rais, Dkt William Ruto kwa kukwepa kuwa na mgombeaji ubunge katika uchaguzi mdogo wa Juja, Kaunti ya Kiambu.

Wamepuuzilia mbali sababu zilizotolewa na viongozi hao wa kikundi cha Tangatanga huku wakisema ni ishara tosha merikebu ya Dkt Ruto ambayo ni chama cha UDA, imeanza kuyumba.Uchaguzi huo umeratibiwa kuandaliwa Mei 18 kufuatia kifo cha Francis Munyua Waititu aliyeugua kansa ya ubongo.

Hata hivyo, Jumatano, Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata alidai kuwa nia kuu ya Dkt Ruto kujiondoa katika kivumbi cha Juja ni heshima kwa Rais ambaye hafai kuaibishwa katika ngome yake ya nyumbani.Aliongeza kuwa Dkt Ruto ameamua kuahirisha ushindani dhidi ya Kieleweke na Handisheki hadi katika kura kuu ya 2022.

“Licha ya kuwa chama cha UDA ndicho maarufu zaidi katika eneobunge la Juja, tulionelea kuwa tupunguze joto la kisiasa katika ngome hii muhimu ya Rais na tumwepeshie aibu ya kuangushwa nyumbani kwake,” akasema.

Kulingana na viongozi wa mrengo wa ‘Kieleweke’, hakuna sababu nyingine ambayo inamchochea Dkt Ruto na wenzake kubadili nia kuhusu kiti cha Juja isipokuwa tu kukwepa aibu ya kubainika wazi kuwa hana ushawishi wa kisiasa kumzidi Rais katika eneo la Mlima Kenya.

“Amekuwa akieneza uvumi kupitia wandani wake Mlima Kenya kuwa yeye ndiye amedhibiti siasa za wenyeji. Amekuwa akijidai kama aliye na ushawishi mkuu katika masuala kama vile ya kupinga urekebishaji katiba na urithi wa urais 2022. Mbona sasa aseme hatawania ilhali ushahidi tosha wa madai yake unaweza tu ukajitokeza kupitia uchaguzi huo?” akahoji mbunge maalum, Bw Maina Kamanda.

Katika chaguzi ndogo zilizopita hivi majuzi, UDA ilifanikiwa kushinda kiti kimoja pekee cha udiwani.Vilevile, Naibu Rais alitangaza awali kuwa hataongoza mrengo utakaofanya kampeni dhidi ya marekbisho ya katiba, baada ya idadi kubwa ya mabunge ya kaunti kupitisha mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kilichoshangaza ni kuwa, katika Kaunti ya Uasin Gishu ambayo ni ngome kuu ya kisiasa ya Dkt Ruto, madiwani waliamua kutojadili wala kupigia kura mswada huo.

“Alikuwa akidai kuwa mchakato wa BBI utazimika kupitia ushawishi wa siasa zake lakini kile tulichoshuhudia ni kushindwa, akawa hoi katika mabaraza yote ya Kaunti za Mlima Kenya na pia kwake nyumbani Uasin Gishu,” akasema Bw Kamanda.

Aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Bw Peter Kenneth alisema kuwa hatua ya UDA kuamua kutokuwa na mgombeaji inaonyesha wazi Rais Kenyatta angali msemaji mkuu wa kisiasa Mlima Kenya.

Hii ni kinyume na msimamo wa baadhi ya viongozi wa Tangatanga ambao husisitiza kuwa Rais amepoteza umaarufu katika ukanda huo ulio ngome yake kuu ya kisiasa.

“Hatuna wakati na siasa za Dkt Ruto wakati baba yetu ni Rais Kenyatta na yuko hai wala hajalemewa kutuongoza kama jamii,” akasema Bw Kenneth.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu (GCE), Bw Wachira Kiago.“Ikiwa Dkt Ruto ana uhakika kuwa ana umaarufu Mlima Kenya, aache kuogopa,” akasema.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: DKT EVANS MAKHULO

Uchumi, sanaa na desturi za kabila la Wadigo uswahilini