Michezo

Wilfred Ndidi afunga pingu za maisha

May 23rd, 2019 1 min read

MASHIRIKA na GEOFFREY ANENE

KIUNGO wa Super Eagles ya Nigeria na klabu ya Leicester City, Wilfred Ndidi sasa ameasi ukapera.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Nigeria, Ndidi na mpenzi wake, Dinma Fortune, walifunga pingu za maisha Jumatano, Mei 22, 2019, jijini Abuja.

“Waliunganishwa katika harusi ya kitamaduni ya kupendeza iliyohudhuriwa na masupasta wengi nchini humo wakiwemo Nwankwo Kanu na Kelechi Iheancho,” vyombo hivyo vimeripoti.

Ndidi na Dinma, ambaye ni mwanafunzi wa elimu ya utabibu, wamekuwa marafiki tangu wakiwa matineja. Wamekuwa wakichumbiana kwa miaka kadha sasa.

Duru zinasema kwamba mwanasoka huyu mwenye umri wa miaka 22 atakatiza shughuli hiyo ya ndoa kwa haraka ili kujiunga na timu ya taifa ya Nigeria kambini inayojiandaa kwa Kombe la Bara Afrika (AFCON) litakalofanyika nchini Misri kutoka Juni 21 hadi Julai 19, 2019.

Fungate

Ndidi amepanga fungate ndefu baada ya kipute hiki cha mataifa 24.

Mchezaji mwenza Iheanacho alichapisha kwenye mtandao wa Instagram picha za harusi hiyo na pia kufichua ilikuwa harusi ya kusisimua.

Nigeria itapimana nguvu dhidi ya Zimbabwe uwanjani Stephen Keshi mjini Asaba mnamo Juni 8 kabla ya kupiga mchuano mwingine wa kirafiki dhidi ya Senegal nchini Misri mnamo Juni 16. Super Eagles iko katika Kundi B pamoja na Guinea, Madagascar na Burundi.