Habari Mseto

William Kingi ahimiza Kenya Power isambaze umeme kupitia nyaya za ardhini

December 6th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

NAIBU Gavana wa Mombasa William Kingi amehimiza kampuni ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power kukumbatia teknolojia ya kisasa.

Aidha Dkt Kingi ameisihi Kenya Power kusambaza umeme kupitia nyaya za ardhini badala ya mfumo wa Millington zinazowaweka wakenya kwenye hatari ya ajali.

“Nimekutana na mkurugenzi wa Kenya Power Bw Bernard Ngugi na tumejadili maswala mengi sana ikiwemo ushirikiano ili kuwekeza katika umeme katika wilaya zote za Mombasa na hasa kuwekeza katika raslimali ya kusambaza umeme kupitia nyaya za ardhini,” alisema Dkt Kingi.

Dkt Kingi alisema kampuni hiyo ikikumbatia mfumo wa kusambaza umeme kupitia ardhini, itadumisha usalama kwani sehemu nyingi zitakuwa na umeme na biashara kunoga hasa wakati huu wa janga la corona ambapo biashara nyingi zimeathirika.

“Kuweka nyaya za umeme ardhini ni mfumo bora zaidi hasa wa kulinda Wakenya kutokana na majanga ya ajali sababu ya nyaya za stima kuning’inia kadhalika itapunguza kupotea kwa umeme mara kwa mara,” alisisitiza.