Bambika

Willy Pozee arejea kanisani baada ya miaka saba!

January 30th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI Wilson Abubakar Radido almaarufu Willy Paul au Willy Pozee, amefichua kwamba kwa miaka saba hajakuwa akikanyaga kanisani.

Alidai sababu ilikuwa kuitwa majina yaliyomsababishia msongo wa mawazo.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Pozee alisema kuwa sasa yuko tayari kusahau matukio yaliyomtendekea. Alisema hayo baada ya kuhudhuria ibada mnamo Januari 28, 2024.

Mwanamuziki huyo aliyevuma kutokana na ngoma yaSitolia’ mwaka 2013 aliepuka kwenda kanisani kwanzia mwaka 2017.

“Sikuwa nikienda kanisani tangu 2017 kwa sababu kanisa lilinifanyia kitu kibaya,” alidai.

Mwazilishi huyo wa Saldido International Entertainment, alisifia ibada kanisani katika mwaka mpya, kuashiria mwanzo mpya.

“Lakini nilihudhuria ibada ya kanisani katika mtaa wa Embakasi na ninahisi nikiwa na furaha sana. Utakuwa mwaka mzuri sana kwa sababu nimeanza kwenda kanisani,” akasema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30, mnamo mwaka 2017 alizua utata mitandaoni baada ya picha yake kuonekana akiwa na mwanamke mmoja kwenye eneo la burudani.

Baadhi ya wafuasi wake na wale wanaoaminika kumwonea kijicho, walianza kumuita majina ya kumchamba.

Walidai hatua hiyo yake ilikuwa sawa na kuingia kwenye tasnia ya muziki wa kilimwengu.

Mwaka wa 2021, alifunguka kwa kugura tasnia ya muziki wa injili hatua hiyo ikimsababishia msongo wa mawazo na mwishowe akavunjika.

“Wengine mnaniuliza kwa nini niliacha Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo… na hata kuniita majina kwa sababu simsifu tena Yesu katika nyimbo zangu. Kulingana na wao mimi ni mbaya sana na kila kitu changu ni kibaya,” akaongeza.