Michezo

Wilshere afadhaishwa na hatua ya West Ham United kumtema

October 6th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Jack Wilshere, 28, amesema kwamba amefadhaishwa pakubwa na hatua ya kutemwa kwake na kikosi cha West Ham United wakati anahisi kwamba angali na mengi ya kuchangia klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Wilshere ambaye ni raia wa Uingereza, aliachiliwa na West Ham mnamo Oktoba 5, 2020, baada ya kuchezea kikosi hicho cha kocha David Moyes jumla ya mechi 19 pekee katika kipindi cha miaka miwili.

West Ham walitamatisha muda wa kuhudumu kwake uwanjani London Stadium akisalia bado na miezi miezi tisa kwenye mkataba wa miaka miwili aliotia saini mnamo 2018.

“Ningali na umri wa miaka 28 pekee. Najihisi kwamba bado nina nguvu ya kucheza. Nina kiu ya kuongoza kikosi kusajili matokeo ya kuridhisha na kupata jukwaa la kujikuza kitaaluma,” akasema.

Wilshere alijiunga na West Ham, ambayo ni klabu aliyoanza kushabikia tangu utotoni, mnamo Julai 2018 kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kuagana na Arsenal.

Hadi kuondoka kwake kambini mwa West Ham, Wilshere alikuwa amechezea kikosi hicho mara moja pekee msimu huu katika ushindi wa 5-1 waliosajili dhidi ya Hull City kwenye Carabao Cup.

Mbali na kushuka kwa ubora wa fomu yake tangu abanduke Arsenal, Wilshere amekuwa mwepesi wa kupata majeraha mabaya ya kumweka nje kwa kipindi kirefu.

Wilshere alichezea Arsenal katika jumla ya mechi 197 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichovunia klabu hiyo ubingwa wa Kombe la FA katika misimu ya 2014 na 2015.

Hadi kufikia sasa, amevalia jezi za timu ya taifa ya Uingereza mara 34 na mchuano wake wa mwisho kuchezea timu hiyo ni katika kichapo cha 2-1 walichopokezwa na Iceland katika hatua ya 16-bora ya Euro 2016 nchini Ufaransa.