Wilson Bii aduwaza Samwel Muchai

Wilson Bii aduwaza Samwel Muchai

Na AYUMBA AYODI

WILSON Bii aliduwaza gunge Samwel Muchai uwanjani Kasarani Jumatatu katika mashindano ya kuchagua kikosi cha Kenya kitakachoshiriki mashindano ya walemavu ya Dubai Grand Prix.

Bii ni mshindi wa medali ya shaba ya Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya mbio za mita 5,000 kitengo cha T11 mwaka 2016 ambacho Muchai alishinda jijini Rio de Janeiro nchini Brazil.

Alitimka umbali huo wa mizunguko 12 na nusu kwa dakika 15 na sekunde 55.5, akilemea majeruhi Muchai kwa mara ya kwanza kabisa. Muchai aliridhika katika nafasi ya pili (15:56.3) nao Rogers Kiprop na Eric Sang wakafuatana katika nafasi ya tatu na nne kwa dakika 16:12.5 na 16:34.4, mtawalia.

“Nafurahia sana kushinda mbio hizi licha ya kuwa hatujakuwa na mashindano kwa muda mrefu kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona,” alisema mkazi wa mji wa Eldoret, Bii.

“Ilikuwa vigumu kushawishi mwelekezi wangu Robert Tarus kuacha familia yake mjini Kericho kuja kunisaidia katika mazoezi na ni heshima kubwa kuwa alikubali mwito wangu,” alieleza Bii, ambaye sasa ametupia jicho kushiriki Olimpiki mwezi Agosti/Septemba baada ya kutimiza muda unaohitajika.

Mashindano ya Dubai yatafanyika Februari 7-14. Ni mojawapo ya mashindano yatakayotumiwa na wanariadha kufuzu kushiriki Olimpiki.

Kamati ya Olimpiki ya Walemavu Kenya (KNPC) iko makini kupeleka washiriki mjini Dubai kwa mashindano hayo pamoja na yale ya Tunisia Grand Prix (Machi 18-20), France Grand Prix (Mei 5-7), Morocco Grand Prix (Juni) na mashindano ya kunyanyua uzani mjini Manchester mwezi Machi.

Bii pia alitwaa taji la mbio za mita 1,500 T11 baada ya Muchai kujiondoa kwa sababu ya jeraha la mguu. Katika kitengo hiki, Bii alitumia dakika 4:23.6 kuibuka mshindi akifuatiwa kwa karibu na Sang (4:29.3) na Kiprop (4:32.7).

“Nasikitika nilipata jeraha la mguu. Nilihisi uchungu sana,” alisema Muchai, ambaye ni mshindi wa medali ya fedha kwenye Olimpiki wa mbio za Beijing mwaka 2008 mbio za mita 1,500 na medali ya dhahabu ya mita 1,500 T11 kutoka Olimpiki za London mwaka 2012.

“Natumai nitapona kwa muda ufaao kabla ya mashindano ya Dubai,” alisema mshindi huyo wa mbio za mita 5,000 T11 za London mwaka 2017 na Dubai mwaka 2019.

Licha ya kuwa hakufanya mazoezi kwa sababu ya masharti makali ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, Sylvia Olero alinyakua taji la kurusha kisahani baada ya kukitupa umbali wa mita 27.43 na kujiweka pazuri kufuzu mjini Dubai.

“Naorodheshwa katika nafasi ya 10 duniani, lakini nataka kurusha kisahani mita 35 mjini Dubai ili niingie mduara wa tano-bora na kujihakikishia tiketi ya kuwa mjini Tokyo,” alisema Olero. “Warushaji tufe wanaoshikilia nafasi 12 duniani wataingia Olimpiki, lakini nitakuwa na uhakika kwa kuandikisha zaidi ya mita 30.”

Wesley Sang aling’ara katika mbio za mita 1,500 T46 alipokamilisha kitengo hicho kwa dakika 4:02.0. Alimaliza mbele ya Stanley Masik na Felix Kipruto waliotimka 4:10.0 na 4:21.5, mtawalia. John Toroitich alitawazwa mshindi wa mita 1,500 T12 kwa muda wa “B” wa dakika 4:02.6 mbele ya Vitalis Kibiwott (4:06.5).

John Kiprotich alibeba taji la mbio za mita 5,000 T12 kwa dakika 15:23.1 huku Bernard Koskei akiridhika katika nafasi ya pili (15:25.6).

Rais wa KNPC, Agnes Aluoch alisema watahitaji Sh7.6 milioni kuwasilisha wanamichezo 30, waelekezi wanane na maafisa 12 kwa mashindano ya Dubai.

“Malengo yetu ni kuingiza timu kambini kuanzia Jumatatu ijayo kwa sababu tunataka Wakenya zaidi wafuzu kushiriki Olimpiki. Wakiwa kambini, hawatakuwa na kisababishi cha kutomakinikia mazoezi kwa sababu hawajayafanya kwa muda mrefu kutokana na janga la virusi vya corona,” alieleza Aluoch na kuongeza kuwa kamati hiyo tayari imeshaandikia Wizara ya Michezo barua ya kuomba ufadhili.

Habari imetafsiriwa na Geoffrey Anene

  • Tags

You can share this post!

Wazazi wahuzunika baada ya watoto wao kukosa fursa ya...

Wamiliki wa shule zilizolemewa na makali ya Covid-19...