Siasa

Wimbi la mbunge Caleb Amisi lafanya mambo magumu kwa Mudavadi, Weta

April 24th, 2024 2 min read

NA EVANS JAOLA

SIKU chache tu baada ya Gavana wa Trans Nzoia kuzindua harakati za msisimko wa kisiasa eneo la Magharibi akisuta Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, mbunge wa Saboti Caleb Amisi ndiye wa hivi punde kuchochea moto huo.

Mabw Mudavadi na Wetang’ula wamejipata pabaya kwa madai kuwa hawajatetea masilahi ya wakazi wa eneo hilo kwa kipindi kirefu.

Gavana Natembeya alikuwa wa kwanza kumshutumu spika Wetang’ula kwa kutowajibika katika uongozi wake, akidai amekuwa anatumia nafasi yake kujinufaisha kibinafsi.

Gavana Natembeya ambaye ameanzisha vuguvugu la ‘Tawe’ linalolenga kuwachochea wakazi wa eneo la magharibi kuasi viongozi wasiotoa usaidizi na kuleta maendeleo, amedai kuwa Mabw Wetangula na Mudavadi wameshindwa kuonyesha ukakamavu na basi hawafai kuwakilisha wakazi wa eneo la Magharibi.

“Mimi nimeanzisha vuguvugu la kukomboa eneo la Magharibi na kuwapa ujumbe wa matumaini na safari hii haiwezi kwama hata nipigwe vita kiasi gani,” gavana Natembeya aliambia Taifa Leo.

Sasa Bw Amisi naye amechochea moto kwa kuanzisha mchakato mwingine wa kuwakosoa Mabw Mudavadi na Wetang’ula.

Bw Amisi anasema wawili hao hawana lolote la kuonyesha jamii ya Mulembe akidai wametumia nafasi zao katika uongozi kujinufaisha kibinafsi.

“Mudavadi amekuwa katika serikali nikiwa na umri wa miaka mitatu na hadi leo hii ninasema kwa mtazamo wangu kwamba hana lolote la kuonyesha watu wa Magharibi. Yeye na Spika Wetang’ula wametuaibisha kama wenyeji wa eneo la Magharibi,” akadai mbunge huyo.

Akizungumza Jumanne mjini Kitale wakati wa kusambaza hundi za basari kwa wakazi, Bw Amisi ambaye ni mwandani wa kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga, alisema anaendelea kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza, akidai imetenga jamii ya Mulembe kwa maendeleo.

Mbunge huyo alisema tayari ameanzisha mchakato wa kuunganisha viongozi chipukizi kutoka eneo hilo ili kuanzisha uongozi mpya wa eneo hilo.

“Sisi tunataka watu wetu wapate viongozi wakakamavu na wanaowajibika kwa wapigakura. Tumeanzisha mchakato mpya wa uongozi ili kutoa matumaini kwa watu wetu,” akasema.

Bw Amisi alishikilia kuwa jamii ya ‘Mulembe’ haijanufaika kutoka kwa serikali licha ya kuwa na idadi kubwa ya wapigakura.

“Sisi tunawaambia viongozi hao wawili kuwa wako na nafasi moja ya mwisho kuongoza jamii yetu na Kenya kwa ujumla. Iwapo mmoja wao hatasimama kama rais mwaka 2027, basi waondoke katika nafasi za uongozi,” Bw Amisi akasema.

Mbunge huyo alisema kuwa yuko tayari kuongoza jamii ya Mulembe iwapo wawili hao watatumia nafasi zao kwa malengo tofauti na matakwa ya kijamii.

Ingawa hivyo, Mabw Mudavadi na Wetang’ula wanashikilia kuwa wao wana tajriba pana na kwamba migawanyiko miongoni mwa wenyeji na wakazi wa Magharibi ni ya hasara kuliko faida.

[email protected]