Habari za Kitaifa

Wimbo mpya siku ya kwenda jela na jinsi alipata umaarufu kwa kumposa mtangazaji Maribe

February 10th, 2024 2 min read

FRIDAH OKACHI NA WANDERI KAMAU

MUDA mfupi baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mfanyabiashara Monicah Kimani, Joseph ‘Jowie’ Irungu, ametoa wimbo mpya wa injili.

Jowie aliweka wimbo huo unaoitwa ‘Nakuabudu’ kwenye mtandao wa YouTube, dakika chache tu baada ya mahakama kumpata na hatia ya kumuua Bi Kimani mnamo Septemba 19, 2018.

 Wimbo huo unaofahamika kama Nakuabudu, wenye ujumbe wa kumtaka Mungu kusikiza kutokana na yanayomkabili ulichapishwa saa nane mchana.

Kwa Muda wa saa mbili wimbo huo ulikuwa umetazamiwa mara 5,138.

“Nakuomba Mungu….Mikononi mwako narejea, Mikononi mwako nalilia,” ujumbe kwenye wimbo huo.

Pia, aliongeza ujumbe wenye tumaini kutoka kwenye biblia.

Zaburi 150:6 “Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Msifuni BWANA.”

Hakimu Nzioka pia aliondoa dhamana ya Jowie na kuamrisha kusalia rumande hadi Machi 8, 2024, atakapohukumiwa.

Mfahamu Jowie Irungu

Alizaliwa na kulelewa Nakuru katika familia ya watu wanne, wavulana wawili na wasichana wawili. Ni mtoto wa pili kwenye familia yake.

Alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenya Polytechnic kinachojulikana kwa sasa Chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya kabla ya kusafiri na kwenda Dubai.

Mwaka 2018, alianza kupata umaarufu alipomchumbia mwanahabari Jacque Maribe baada ya kupakia picha na video hizo kwenye mtandao wa Instagram.

Pia, alifahamika na marafiki wa karibu kuwa alifanya kazi ya kutoa ulinzi huko Dubai kwenye familia za kifalme za kiarabu na kuwa na mpango wa kufungua kampuni ya aina hiyo nchini Kenya.

Mauaji ya Monica Kimani yalimfanya kufahamika na wengi baada ya kukamatwa na kuzuiliwa kenye magereza ya Kamiti-Manyani na kuachiliwa baada ya mwaka mmoja na miezi sita.

Mwaka 2020 aliachiliwa kwa dhamana na kurejea kwa wazazi wake. Kisha akahamia kwa mpenzi mpya Eleanor ‘Ella’ Musangi ambaye ni mwanamitindo.

Mwaka huo, wakati wa mawimbi ya Covid 19, Jowie alisema ameokoka na kuwa mwanamuziki wa injili na kutoa nyimbo tatu kabla ya kupumzika.

Desemba 2020, alikatiza mahusiano yake na Eleanor.

Desemba 15, 2023 alitoa wimbo wa tano na dakika chache baada ya kupatikana na hatia kupakia wimbo mwingine.