Wingu jeusi lakumba mustakabali wa kisiasa wa Mudavadi baada ya kushindwa katika ngome yake

Wingu jeusi lakumba mustakabali wa kisiasa wa Mudavadi baada ya kushindwa katika ngome yake

NA CHARLES WASONGA

MUSTAKABALI wa kisiasa wa kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi umo hatarini baada ya chama hicho Jumanne wiki jana kushindwa vibaya katika ngome yake ya kaunti ya Vihiga.

Bw Mudavadi, ambaye mmoja wa vinara wakuu katika muungano wa Kenya Kwanza, alishindwa kutimiza ahadi yake ya kuvutia asimilia 90 ya kura za urais kwenye kapu la Naibu Rais William Ruto.

Kulingana na matokeo ya kura za urais, mgombea urais wa chama cha muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga alizoa kura 143,371 kutoka kaunti ya Vihiga, idadi inayowakilisha asilimia 63.7 ya kura zilizopigwa.

Kwa upande mwingine, Dkt Ruto aliyeungwa mkono na Bw Mudavadi, alipata kura 79,722 pekee, sawa na asilimia 35.4 ya kura zilizopigwa.

Aidha, ANC ilishindwa kutamba katika eneo bunge lake la Sabatia baada ya kupoteza kiti kwa mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mgombeaji wa UDA Clement Sloya alizoa kura 23,925 huku Dkt Emmanuel Ayodi wa ANC akapata kura 10,539 pekee.

Nacho kiti cha eneo bunge la Luanda kilitwaliwa na Dick Maungu wa chama cha Democratic Action Party (DAP-K) ambacho ni chama kimojawapo cha vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

ANC ilishinda viti vitatu vya maeneo bunge kati ya vitano katika kaunti ya Vihiga.

Viti hivyo ni; Emuhaya kilichohifadhiwa na Omboko Milemba, Vihiga (Ernest Kagesi) na Charles Gimose (Hamisi).

Chama cha ODM pia kilifaulu kuhifadhi kiti cha ugavana kinachoshikiliwa na Dkt Wilbur Otichillo na kikaipokonya ANC kiti cha useneta kupitia ushindi wa Godffrey Osotsi.

Bw Mudavadi pia alipata pigo kubwa katika uchaguzi wa udiwani baada ya ODM kushinda viti 10 huku ANC ikishinda viti sita pekee katika ngome hiyo ya Vihiga.

Hii ina maana kuwa ODM itadhibiti bunge la kaunti ya Vihiga huku ikiendesha serikali ya kaunti hiyo kupitia Gavana Dkt Otichillo, kinyume kabisa la matarajio ya Bw Mudavadi.

Kulingana na mkataba wa makubaliano kati ya vyama vya UDA, ANC na Ford Kenya, Mbw Mudavadi na Moses Wetang’ula walihitaji kumzolea Dkt Ruto asilimia 70 za kura za urais kutoka magharibi mwa Kenya ili vyama hivi vipate mgao wa asilimia 30 ya nyadhifa kuu katika serikali ya Kenya Kwanza.

Lakini akihutubu katika mkutano wa kampeni katika uwanja wa michezo wa Hamisi mnamo Julai 31, 2022, Bw Mudavadi aliahidi, mbele ya Dkt Ruto, kwamba angefaulu kuzoa asilimia 90 ya kura zote 310,000 za urais katika kaunti yake ya Vihiga.

“Mimi na Wetang’ula tuko hapa. Ingo (nyumbani) imekubali. Asilimia 70 ni kidogo. Tutaleta asilimia 90 kutoka hapa Vihiga na eneo la magharibi kwa ujumla,” Bw Mudavadi akasema.

Hii ni baada ya Dkt Ruto ambaye alikuwa akiendesha kampeni katika kaunti ya Vihiga kudai kuwa asilimia 70 za kura zilizopendekezwa katika mkataba wa makubaliano ya Kenya Kwanza, “ni kidogo sana”.

Lakini ilivyodhihirika katika matokeo ya uchaguzi wa urais magharibi mwa Kenya, Mbw Mudavadi na Wetang’ula walishindwa kutimiza ahadi hiyo.

Isitoshe, hata katika kaunti ya Bungoma ambako Dkt Ruto alikuwa anaongoza kulingana na matokeo ya awali, Naibu Rais aliweza kupata asilimia 63.4 ya kura za urais.

Hii inaashiria kuwa Bw Wetang’ula pia alishindwa kumwezesha Dkt Ruto kupata angalau asilimia 70 ya kura za urais katika ngome yake.

Hata hivyo, chama chake cha Ford Kenya kilidhihirishwa ubabe wake katika kaunti hiyo kwa kushinda viti vinne vya ubunge kati ya tisa, kiti cha ugavana kupitia Spika wa Seneti Kenneth Lusaka na kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Kike kilichohifadhiwa na Catherine Wambilyanga.

Bw Wetang’ula pia alifaulu kuhifadhi kiti chake cha useneta wa Bungoma, na kupata nafasi ya kuhudumu kwa muhula wa tatu.

Lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema Bw Mudavadi ndiye alipata ‘majeraha’ makubwa kisiasa katika uchaguzi uliopita.

“Ni wazi kuwa Bw Mudavadi ndiye alipoteza pakubwa sio tu katika kaunti yake ya Vihiga bali katika eneo zima la uliokuwa mkoa wa magharibi. Hii ni kwa sababu chama chake cha ANC kilifanya vibaya zaidi kwa kushinda viti vitano pekee vya ubunge tofauti na uchaguzi mkuu wa 2017 kiliposhinda viti 13,” anasema Bw Martin Andati.

“Hii ina maana kuwa kwa serikali ya Dkt Ruto itarajiwe kwamba Bw Mudavadi hatapata kiti cha Mkuu wa Mawaziri alichoahidiwa katika mkataba wa Kenya Kwanza. Hili ni pigo kubwa zaidi,” akaongeza.

Sababu ni kwamba mkataba huo una kipengele kinachosema kuwa endapo ahadi zilizotolewa humo hazitatimizwa, suala hilo litaangaliwa upya endapo Kenya Kwanza itashinda urais.

Kando na viti vitatu ambavyo ANC ilishinda katika kaunti ya Vihiga, chama hicho pia kilishinda viti viwili vya ubunge katika kaunti ya Kakamega. Hivi hivyo, ni Malava kilichohifadhiwa na Bw Malulu Injendi na Shinyalu kilichomwendea limbukeni katika siasa, Fredrick Lusuli. ANC haikushinda viti vyovyote vya ubunge katika kaunti za Busia na Bungoma.

Bw Mudavadi amekuwa katika “baridi ya siasa” kwa miaka 20 tangu 2002 alipovuliwa wadhifa wake wa ubunge wa Sabatia baada ya kushindwa na Moses Akaranga katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Wakati huo alikuwa pia akihudumu kama makamu wa rais, wadhifa ambao alitarajiwa kuhifadhi endapo Rais Uhuru Kenyatta angeshinda urais mwaka huo.

Lakini mambo yalimwendea mrama kwani Bw Kenyatta alishindwa na Rais wa zamani Hayati Mwai Kibaki katika uchaguzi wa mwaka huo.

Tangu wakati huo Bw Mudavadi hajawahi kushikilia kiti chochote cha kuchaguliwa.

Aliwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2013 lakini akafeli kwa kushikilia nafasi ya tatu nyuma ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Mshindi wa kiti cha urais Dkt William Ruto atoa hotuba...

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa lasagna ya mboga mboga

T L