WINNIE ONYANDO: Simu ya mwenzio sumu

WINNIE ONYANDO: Simu ya mwenzio sumu

Na WINNIE ONYANDO

Simu ni gajeti ndogo ila huweza kusababisha mengi kati ya wapendanao. “Mke wangu anashinda kwa simu kila mara, hanipi umakini wake hata ninapomwongelesha,” aliteta Michael, ambaye ni mkazi wa Huruma, Nairobi.

Matumizi mabaya ya simu inaweza kujenga ukuta mrefu kati ya wanandoa na hata kufikia katika hatua ya kuvunjika kwa ndoa hizo.

Wengi waliooana hupendelea kuepuka kushika simu ya mwenzake kwa kuwa ni pilipili. Unaposhikwa na tamaa ya kushika simu ya mume au mke wako, utayakuta sunami itakayokukwaza moyo bure.

“Epuka sana kugusa simu ya mke au mume wako, ione kama janga hatari,” Benter, mshauri mashuhuri wa mapenzi alishauri.

Wengi walipinga kauli hiyo ya Benter wakisema kuwa, “lazima niwe huru kugusa simu ya mke au mume wangu wakati wowote, sisi ni mwili mmoja. Huenda akawa na mpango wa kando na aniletee magonjwa.”

Kila mmoja ana huru kuweka nywila anayopenda katika simu yake, bali hili lisikuwe chanzo cha kutokuwa mwaminifu katika uhusiano.

Kama wanandoa, ni jukumu la kila mmoja kujichunguza na kuwa mwaminifu

“Kama watu wanaopendana na kujaliana, sioni haja ya kuweka nywila kwenye simu, tunafaa kuwa huru kugusa simu ya wapenzi wetu bila kuwa na kizuizi,” Stacy, ambaye ameolewa, aliandika katika mtandao wake wa Facebook.

Kunazo sababu kadha wa kadha ambazo huweza kumfanya mtu kuinamia simu na hata kucheka ovyo ovyo akiwa na simu.

Huenda mkewe Michael yupo katika shughuli zake za kibinafsi ambazo hazimhusu mumewe.b Pengine anafurahishwa tu na watu kwenye mitandao na hili lisimtie Michael wasiwasi.

Hivyo mtu asifikirie kuwa ikiwa mwenzake anatumia simu sana na kuipa umakini wake wote ni kuwa anachepuka. La! Mengi yanawezatendeka ikiwa mmoja kati ya wanandoa anatumia simu sana.

Ikiwa wawili hao wanatumia simu muda mwingi sana, huenda wakapuuza mahitaji ya watoto nyumbani na kuwafanya waathiriwa kujitenga na kuhisi upweke.

Wawili hao pia huenda wakatafuta njia mbadala ya kutimiza hamu na mahitaji yao ya kibinafsi. Huenda ikawa kwa kutazama video vya ponografia.

Mambo kama hayo yanapotokea kati ya wapenzi basi ishara za kutoaminiana, kutoridhishana, upweke, kutojaliana hujidhihirisha.

Kama wapenzi ni vyema kukaa na kujadiliana kuhusu misingi ambayo mnataka itawale uhusiano wenu kabla hamjaamua kufunga pingu za maisha.

Kila mmoja katika uhusiano huwa na matarajio tofauti na mwengine, hivyo mnapojadiliana mnapata kujenga ukuruba na hata kuweka msingi unaofaa ya kutawala uhusiono wenu.

Mnapoamua kuwa hakuna kushika simu ya mwenzako, basi usishikwe na kiherehere ya kugusa simu ya mwenzako hata siku moja kwa kuwa itakuwa sumu kwako.

You can share this post!

Klabu ya Masud Juma yaendelea kuzama Ligi Kuu Morocco

SIASA NI UTUMWA TU – KIRAITU MURUNGI