Habari

Wiper: Kalonzo sasa hataapishwa

February 25th, 2018 1 min read

Na KITAVI MUTUA

VIONGOZI wa chama cha Wiper wameondolea mbali uwezekano wa kinara mwenza wa NASA Kalonzo Musyoka kuapishwa kuwa Naibu wa Rais wa Wananchi.

Wakiongozwa na seneta wa zamani Johnstone Muthama na aliyekuwa waziri Titus Mbathi, viongozi hao walimshauri Bw Musyoka kwamba kuapishwa kwake hakutakuwa na faida yoyote kwake, kisiasa.

Badala yake wamemtaka kuelekeza nguvu na rasilimali kuimarisha chama cha Wiper ili kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

“Mbona uapishwe ilhali hautapewa mamlaka yoyote ambayo yataleta faida kwa wafuasi wako baada ya halfa hiyo,” Mbw Mbathi akamwambia Bw Musyoka mbele yake katika mkutano wa viongozi wa Ukambani katika mkahawa wa Stoni Athi Resort, kaunti ya Machakos.

Alilalamika kuwa Bw Musyoka ametusiwa hadharani na wafuasi wa ODM kwa kutohudhuria halfa ya kuapishwa kwa Raila Odinga ihali hakuna faida yoyote iliyotokana na shughuli hiyo.

Kauli sawa hiyo ilitolewa na Bw Muthama, akisema yeye pia aliamua kutohudhuria hafla hiyo ilhali alikuwa mwanachama wa kamati andalizi ya shughuli hiyo.
Alisema yeye pia alikwepa hafla hiyo ili kulinda masilahi ya chama cha Wiper.