Wiper kumtia adabu Muthama kupitia mke waliyeachana

Wiper kumtia adabu Muthama kupitia mke waliyeachana

Na PIUS MAUNDU

CHAMA cha Wiper kimepanga kumsimamisha mwanasiasa mwanasiasa Agnes Kavindu, aliyekuwa mke wa Seneta wa zamani wa Machakos, Johnstone Muthama, kuwania Useneta wa Machakos katika uchaguzi mdogo wa Machi 23.

Kiti hicho kilisalia wazi baada ya mauti ya aliyekuwa Seneta Boniface Kabaka mnamo Disemba mwaka jana akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi.

Ingawa Bi Kavindu hajatangaza chama atakachotumia, duru zilifichua kuwa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka yuko tayari kumpa Bi Kavindu tiketi ili kumdhibiti kisiasa Bw Muthama.

Bw Muthama aliunda chama cha United Democratic Alliance na anarindima ngoma ya Naibu Rais Dkt William Ruto eneo la Ukambani. UDA ilimtangaza aliyekuwa Naibu Gavana Bernard Kiala kuwania kiti hicho.

Wikendi iliyopita, Bi Kavindu alitangaza kuwa yupo kiny’ang’anyironi huku zaidi ya wawaniaji 20 pia wakijitokeza kuweka wazi azma yao.

Bi Kavindu ambaye aligombea kiti cha Mwakilishi wa Wanawake, Machakos 2017 na kubwagwa na Joyce Kamene wa Wiper, aliambia Taifa Leo kuna uwezekano atatafuta tikiti ya Wiper.

Uchaguzi huo pia umetajwa na wadadisi wa kisiasa kama jukwaa la ubabe kati ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Maendeleo Chap Chap Dkt Alfred Mutua pamoja na Bw Muthama.

MCC tayari imempa tiketi aliyekuwa Waziri wa Maji wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, Bw Mutua Katuku.

You can share this post!

Sonko agundua kumbe Nairobi ina wajanja kumliko

Vikosi 14 vya EPL vilivyotinga raundi ya nne FA