Habari

Wiper kutangaza mwenyekiti mpya mwishoni mwa Julai

July 10th, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha Wiper kimetangaza kwamba kitatangaza mwenyekiti mpya mwishoni mwa mwezi huu wa Julai kurithi nafasi hiyo kutoka kwa Gavana wa Makueni, Profesa Kivutha Kibwana.

Kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Chama ulioandaliwa Jumatano katika makao yake makuu mtaani Karen, Naibu Mwenyekiti, Mutula Kilonzo Jnr amepuuza taarifa ambazo zimekuwa zikienea katika vyombo vya habari kwamba waziri wa zamani Ali Mwakwere tayari amepokezwa wadhifa huo.

Bw Mutula amesema Wiper itaandaa warsha hiyo mjini Naivasha ambapo jina la mwenyekiti mpya litatangzwa na pia mikakati ya kuvumisha chama hicho itapangwa na kuwekwa bayana.

“Tumekutana leo (Jumatano) ili kujadiliana kuhusu uongozi wa chama. Tumekubaliana kuandaa warsha mwishoni mwa mwezi huu (Julai) ili kutangaza mwenyekiti mpya. Ripoti ambazo zimekuwa zikienea kwamba tumemchagua Balozi Mwakwere kama mwenyekiti wa chama ni uongo na nafasi hiyo itajazwa wakati wa warsha hiyo,” akasema Bw Kilonzo Jnr.

Naye Kalonzo amebainisha lengo la warsha itakayoandaliwa.

“Tutaenda kwenye warsha hiyo kubadilisha uongozi na iwapo Prof Kibwana anataka kuhudhuria mkutano huo amekaribishwa japo ni wazi kwamba amekuwa akihepa mikutano mingi ya chama,” akasema Bw Kalonzo.

Prof Kibwana ambaye chama chake cha Muungano kiliingia katika ndoa ya kisiasa na Wiper kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2017, amekuwa na uhusiano mbaya na kigogo wa siasa za Ukambani, Kalonzo Musyoka ambaye pia ni kiongozi wa Wiper na mbunge wa zamani wa Mwingi Kaskazini.

Chama hicho pia kimesifu kuteuliwa kwa Bw Musyoka kama Balozi wa Amani nchini Sudan Kusini.

Uteuzi ulifanywa na Rais Uhuru Kenyatta, wiki chache zilizopita.