Habari Mseto

Wiper yashirikiana na Jubilee kujumuisha Momanyi kwa PSC

February 21st, 2018 1 min read

Mbunge wa Borabu Ben Momanyi aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper. Picha/ Maktaba

Na CECIL ODONGO

MJADALA mkali ulichacha bungeni Jumatano mchana wakati wa kujadili majina ya wanachama waliopendekezwa kuhudumu kwenye Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Majina ya wanachama hao yanatarajiwa kupigiwa kura na kuidhinishwa na bunge mnamo Alhamisi ili tume ianze kazi.

Ushirikiano usiokuwa wa kawaida kati ya chama cha Jubilee na kile cha Wiper ulidhihirika wazi kwenye mjadala huo uliohusu kujumuishwa kwa Mbunge wa Borabu Ben Momanyi aliyechaguliwa kwa tiketi ya Wiper.

Kiongozi wa wachache bungeni John Mbadi alimweleza spika kwamba Muungano wa NASA uliamua kumpendekeza Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr kuchukua nafasi ya seneta wa Vihiga George Khaniri kama njia ya kuridhia uwakilishi wa Wiper.

Hata hivyo Kiongozi wa wengi Bungeni Aden Duale alipinga ombi hilo na hata kujumuisha jina la mbunge wa Borabu Ben Momanyi miongoni mwa waliopendekezwa na chama cha jubilee kama NASA hawakutaka kumpendekeza.

Bw Duale alisisitiza kwamba chama cha Wiper kina asilimia tano kwenye uwakilishi bungeni na kisheria wanastahili nafasi moja kwenye tume ya PSC.

Katika kile kilichonyesha wazi tofauti kati ya wiper na ODM, Mbunge wa Kitui ya kati Makali Mulu aliunga uteuzi wa Bw Momanyi.

Akitoa uamuzi wake kuhusu swala hilo spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi aliunga kujumuishwa kwa Ben Momanyi akifafanua kihesabu asilimia ya kila chama kwenye mungano wa Nasa katika kupata nafasi kwenye PSC.

Alisisitiza kwamba mfumo huo ndio ulitumiwa kuwachagua wawakilishi wa nchi kwenye bunge la Afrika Mashariki na ungebadilishwa tu iwapo wabunge wangepitisha sheria nyingine.

Spika Muturi alikomesha mjadala huo na hata kumkomesha Mbunge wa Uriri Mark Nyamita aliyesimama kuupinga uamuzi huo.