Habari MsetoSiasa

Wiper yavunja mkataba na Nasa, yaingia Jubilee rasmi

July 21st, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha Wiper kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka, kimeamua kuunda muungano rasmi na Chama cha Jubilee.

Hatua hii ni kumaanisha kuwa, Wiper itakuwa chama cha kwanza kuhama Muungano wa National Super Alliance (NASA) na kufungua mlango wa muungano huo kuvunjwa.

Makubaliano yaliyotumiwa kuunda muungano huo huhitaji vyama vitatu kujiondoa ndipo iwe kwamba muungano umevunjika.

Hatua hii inajiri mwezi mmoja baada ya Wiper kutia sahihi mkataba wa ushirikiano na Jubilee.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wiper Judith Sijeny alisema Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho (NEC) ilitambua kwamba Muungano wa NASA umesambaratika.

Wiper ni chama tanzu katika muungano huo unaoshirikisha vyama vya Orange Democratic Movement (ODM) cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, Amani National Congress (ANC) cha aliyekuwa makamu wa Rais Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha Seneta wa Bungoma Moses Wetangula.

Ingawa chama cha ODM kinashirikiana na Jubilee nje na ndani ya bunge, hakina mkataba wowote wa ushirikiano au kuungana na chama hicho tawala.Bi Sijeny alisema mkutano maalumu wa wabunge wa chama utaitishwa kuidhinisha azimio la NEC la kuungana na Jubilee rasmi.

Katika mkutano wa jana, Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho lilikubali ripoti ya kamati ya nidhamu iliyopendekeza kutimuliwa kwa aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama.

Bw Muthama ametofautiana na chama hicho kwa kuungana na Jubilee na ametangaza kuwa anashirikiana na Naibu Rais William Ruto ambaye wandani wake wametengwa katika chama cha Jubilee.

Mwanasiasa huyo alikataa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama na kutangaza kuwa alikihama alipokataa kugombea useneta wa Machakos 2017.

Bi Sijeny alisema Wiper itamwandikia barua msajili wa vyama vya kisiasa ili Muthama ondolewe kama mwanachama wake.