Habari za Kaunti

Wito busara itumike kufanikisha mradi wa kawi ya nyuklia

January 4th, 2024 2 min read

NA ALEX KALAMA

BAADHI ya wakazi wa Matsangoni katika Kaunti ya Kilifi, wanaitaka serikali kutuma timu katika eneo hilo na kutoa taarifa kamili kuhusu ujenzi wa mradi wa kawi ya nyuklia, ulioratibiwa kuanza kujengwa kuanzia mwaka 2026 katika eneo hilo.

Kulingana na baadhi ya wakazi wa eneo hilo, baadhi ya viongozi wamelaumiwa kutokana na kuenea kwa uvumi mwingi kuhusu mradi huo huko mashinani.

Wanadai viongozi wameendeleza pingamizi ili kuhakikisha mwananchi wa kawaida hapati taarifa sahihi.

Wakiongozwa na Mzee Bahati Karisa, ambaye ni mkazi wa Uyombo, wakazi hao wanasema kuwa pingamizi zinazoendeshwa na mashirika na viongozi mashinani, zimekuwa kikwazo kikuu kwa wenyeji kupata taarifa hizo.

Hali hii imefanya baadhi ya raia kuwatimua baadhi ya maafisa wa mamlaka ya kawi ya nyuklia nchini (NUPEA) wanapofika mashinani kuendeleza hamasisho kuhusu mradi huo wa kawi ya nyuklia.

“Wale viongozi wachache ambao sasa wanaongoza makundi ya wale wanaopinga, hawataki kabisa hata mwananchi apewe hamasisho. Hapo sasa ndipo palipo na kikwazo kikubwa kwa sababu huyo mwananchi anakosa mahali pa kushikilia, na anakosa kujua ulipo ukweli,” akasema Bw Karisa.

Kwa upande wake, Mzee Clapaton Kazungu anasema kuwa kando na kutatua utata wa umiliki wa mashamba eneo hilo, ni sharti kamati ya eneo hilo ipewe fursa ya kusafiri hadi katika mojawapo ya mataifa yenye mradi sawa na huo kwa lengo la “kujionea usalama wa mradi huo kwa wenyeji na athari zake katika maisha ya mwananchi kabla ya mradi huo kuanza.”

“Lazima wachukue jukumu la kupeleka watu, kwa mfano hadi nchini Korea au kwingineko kuliko na miradi kama hiyo. Watu wakipelekwa kule kuonyeshwa mradi wa kawi ya nyuklia, watajua vile ambavyo wanaishi na ule mradi,” akasema Bw Kazungu.

Hata hivyo, Mama Kitsaka Kiraho, ambaye ni mzee wa mtaa wa Uyombo Madeteni B, amesisitiza haja ya serikali kuendelea mbele na utafiti wake ili kufanya uamuzi wa iwapo mradi huo utajengwa katika Kaunti ya Kilifi au kaunti jirani ya Kwale.

“Mfano mzuri ni majuzi tu hapa Kenya umeme ulipotea kila sehemu ya nchi. Kenya nzima umeme ulipotea. Je, kama mtambo ule ungekuwa si ungetusaidia? Kuna wengi walipata hasara. Hata mimi niko na mtoto wangu aliyepata hasara baada ya samaki kilo 100 kuoza kwa sababu ya umeme kupotea na hivyo akalazimika kutupa,” akasema Bi Kiraho.

Akaongeza: “Mimi ningeomba wafanye huu utafiti kwa haraka sana kwa sababu tunataka kuepuka haya mambo ya umeme kupoteapotea kila mara.”