Habari

Wito jopo liundwe kuchunguza vifo vya wanafunzi 14

February 7th, 2020 2 min read

DERICK LUVEGA NA WANDERI KAMAU

SWALI “ni nini kilichosababisha vifo vya wanafunzi 14 wa shule ya Msingi ya Kakamega” ndilo lililotawala vinywani mwa waombolezaji mbalimbali waliofika kwenye ibada ya wafu iliyofanyiwa wanafunzi hao Ijumaa.

Ni kitendawili ambacho hadi sasa kimekosa mteguzi tangu wanafunzi hao kukutana na mauti hayo mnamo Jumatatu.

Katika juhudi za kulifumbua fumbo hilo, viongozi mbalimbali wa kisiasa kutoka eneo la Magharibi waliohutubu katika ibada hiyo mjini Kakamega, walitoa wito kuwa uchunguzi uendeshwe na jopo maalum bali si polisi.

Wanaamini kuwa polisi hawana uwezo wa kutosha kuweza kubaini kiini cha mauti hayo.

Wwanataka jopo maalum libuniwe kufanya uchunguzi ili kubaini kilichosababisha mkasa uliotokea katika Shule ya Msingi ya Kakamega, Kaunti ya Kakamega, ambapo wanafunzi 14 waliaga dunia.

Wanafunzi hao walifariki mnamo Jumatatu kwenye mkanyagano uliotokea walipokuwa wakitoka katika madarasa yao kuelekea nyumbani.

Viongozi hao, akiwemo kinara wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi, Bw Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), Seneta Cleophas Malala (Kakamega) na aliyekuwa Seneta wa kaunti hiyo Dkt Boni Khwalwale, walisema kuwa hilo ndilo litakalotoa jibu kuhusu kilichosababisha mkasa huo.

Wakihutubu Ijumaa kwenye misa ya wafu kuwakumbuka wanafunzi hao katika Uwanja wa Bukhungu, Kakamega, viongozi walisema kwamba huenda uchunguzi wa polisi usitoe majibu kamili kuhusu kiini cha ajali hiyo.

“Polisi hawawezi kuchunguza kisa kama hiki. Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji anapaswa kubuni jopo la uchunguzi kubaini ikiwa kuna watu waliohusika. Hilo litahakikisha wale watakaopatikana kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria,” akasema Bw Wetang’ula.

Kwa upande wake, Bw Mudavadi alisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee itakayohakikisha kuwa mkasa huo hautokei tena.

“Wizara ya Elimu inapaswa kutathmini kwa kina tukio hili. Lazima kanuni zote zilizowekwa zitimizwe kabla ya mtu kupewa cheti cha kuendesha taasisi yoyote ya umma,” akasema.

Gavana Wycliffe Oparanya alisoma majina ya wanafunzi hao, huku akiwarai wananchi kuiombea kaunti hiyo kwani imekumbwa na misururu ya maafa tangu mwaka 2014.

“Tunawaomba kuiweka Kaunti ya Kakamega kwenye maombi,” akasema.

Katibu wa Elimu Dkt Belio Kipsang alisema kwamba kila familia ya mwanafunzi aliyefariki imepewa Sh100,000 na serikali ili kugharamia mazishi.

Misa ilifanywa kuwakumbuka wanafunzi 13, baada ya mwanafunzi mmoja kuzikwa Jumatano kulingana na imani ya Kiislamu.

Familia za waathiriwa zilianza kuwasili katika uwanja huo asubuhi, huku hali ya huzuni ikitanda.

Majeneza yaliyokuwa na miili hiyo yaliwekwa kando kando chini ya hema maalum.