Habari Mseto

Wito kaunti iondoe dampo la Mwakirunge

October 25th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

WAKAZI wa Mwakirunge mjini Mombasa wanaitaka serikali ya kaunti iliondoe dampo huko, wakisema wameanza kuathiriwa na uvundo na moshi.

Jalala hilo lilihamishiwa Mwakirunge ambako kuna makazi ya zaidi ya watu 2,000 baada ya kuondolewa eneo la Kibarani.

Taifa Leo ilipozuru pahala hapo, iliwaona watoto wenye umri mdogo wakichokora sehemu hiyo bila kinga yoyote mikononi wala miguuni.

“Tumejaribu kuwakataza kufanya biashara hiyo na kurudi shuleni lakini hali duni ya maisha inawarudisha sehemu hiyo,yeyote anayenunua bidhaa hizo kwa watoto hao lazima achukuliwe hatua,” alisema mtetezi wa haki za watoto Bi Grace Ogembo.

Bi Ogembo alisema kuna visa vya watoto kuchomeka na kemikali, kudungwa na sindano,na hata kupata maambukizi ya magonjwa ya kuharisha na yale ya ngozi.

Bi Kache Mupa mkazi wa eneo hilo alisema jaa hilo linahatarisha afya za wenyeji na aliiomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kulihamisha au kulizungushia ukuta ili kuwazuia watoto kulifikia.

Mbali na matatizo ya kiafya yanayoletwa na jaa hilo wakazi pia wanasema jaa hilo linarudisha nyuma maendeleo ya eneo hilo.

“kuna watu walikuwa wameanza kuwekeza katika eneo hili lakini kufuatia harufu ya uvundo barabara zilizozibika kufuatia utupaji ovyo wa taka kumewafanya baadhi yao kuuza mashamba yao na kuhama sehemu zengine,”alisema.

Alisema plastiki na kemikali zinazomwagika katika eneo hilo pia zimechangia mazao yao kuzorota,wakisema wanakadiria hasara.

Bw Elias Mwandembo mkulima katika eneo hilo alilalamikia njia zisizopitika kufuatia madereva wanaoendesha magari ya taka wazembe wanaomwaga taka kandoni mwa barabara.

“Milima hiyo ya taka humwaika barabarani, hivyo inakuwa vigumu kupisha gari au hata kwa wanaotembea kwa miguu,” alisema.

Magari yagongana

Aliongezea kuwa wameshuhudia visa kadhaa vya magari kugongana kufuatia ukungu unatokana na moshi baada ya maafisa wa kaunti hiyo kuteketeza taka moto ili kuzipunguza.

Barabara hiyo inaunganisha Mombasa na Kaloleni. Hiyo huwa njia mbadala kwa magari ya kutoka Nairobi nyakati kuna msongamano wa magari katika barabara kuu ya Mombasa Nairobi.

“Hapa kuna taka za kila aina, kwanza moshi wake unasababisha wakazi kukohoa na kushikwa na mafua yasiyoisha, pili moshi unapofuka madereva hawaonani hivyo kusababisha ajali,” alisema.

Bw Hamisi Katana alieleza wanahofia kudorora kwa usalama kufuatia vijanawanaotumia madawa ya kulevya kutumia jaa hilo kama maficho yao.

“Baada ya kutumia madawa akili huharibika,tunahofia mateja hawa kuanzisha tabia za kunajisi wanawake wetu na watoto,”alisema.

Wakazi hao walipendekeza serikali kunyunyizia madawa mara kwa mara kufukuza nzi wanaoleta magonjwa ya macho na kipindupindu.

Aidha walitaka serikali kueka afisa atakae hakikisha takataka zinamwagwa ndani ya shimo kama ilivyoagizwa.

Aidha walisema serikali haijaweka mtambo wa kuchoma taka kama walivyowaahidi hapo mwanzo na badala yake wanazichoma.