Habari Mseto

Wito serikali idhibiti maajenti wanaowapeleka Wakenya kufanya kazi Uarabuni

September 29th, 2020 1 min read

Na Winnie Atieno

MADIWANI katika Kaunti ya Mombasa wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuweka mikakati ya kudhibiti kampuni na maajenti wanaowasajili wakazi kufanya kazi nchi za Uarabuni.

Walitaka pia serikali kuu kuidhinisha sera kali za leba ili kuwalinda Wakenya dhidi ya mateso uarabuni.

“Sera zilizoko ni nzuri lakini hazisuluhishi matatizo ya dhuluma kwa Wakenya wanaofanya kazi Uarabuni. Kampuni husika zinafaa kuchukuliwa hatua endapo Mkenya yeyote atateswa au kudhulumiwa wakiwa Uarabuni,” alisisitiza mwenyekiti wa kamati ya Leba katika bunge la Mombasa, Bw Renson Thoya.

Bw Thoya alisema kampuni nyingi huajiri Wakenya wasiokuwa na tajriba hivyo basi kuwa rahisi kuwanyanyasa.

Hata hivyo, aliwataka wawekezaji wa sekta hiyo kuhamasisha Wakenya dhidi ya ulanguzi wa binadamu, ukiukaji wa sheria za leba na kampuni ghushi zinazosafirisha Wakenya Uarabuni wanakoenda kutesekea.