Wito serikali ifanye kila iwezalo uchaguzi usiyumbishe utalii

Wito serikali ifanye kila iwezalo uchaguzi usiyumbishe utalii

NA KALUME KAZUNGU

WADAU wa utalii wameitaka serikali kuweka mikakati ya kulinda biashara zao dhidi ya athari zozote katika msimu mzima wa siasa za uchaguzi wa Agosti.

Baada ya kuathiriwa pakubwa na janga la corona, wadau hao sasa wameonya kuwa joto la kisiasa nchini litasambaratisha zaidi sekta hiyo siku za hivi karibuni, ikiwa sekta hiyo haitatiliwa maanani.

Wakizungumza katika Kaunti ya Lamu, wadau hao, wakiwemo wamiliki wa hoteli, vijana wa huduma za kutembeza watalii ufuoni, manahodha wa boti za kuendesha watalii na wafanyabiashara wa maduka ya mapambo, walisema idadi ya watalii wanaozuru eneo hilo imeanza kudidimia, hasa tangu kampeni za kisiasa zilipoanza kushika kasi nchini.

Baadhi ya sehemu zinazotoa huduma za watalii kwenye miji ambayo ni ngome ya kitalii, ikiwemo Shella na mji wa kale wa Lamu, zimefungwa kutokana na kuadimika kwa wateja.

Bw Lali Shee, ambaye ni mmiliki wa hoteli mjini Lamu, alisema amelazimika kufunga hoteli yake na kuwatuma wafanyakazi zaidi ya 10 nyumbani hadi baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

“Msimu huu wa watalii wachache huwa pia tunapata wageni, japo kidogo kwa siku. Cha ajabu ni kwamba tangu kampeni za kisiasa zilipoanza kunoga, wale watalii wachache tuliotegemea wamehama ilhali wengine waliopanga kuja Lamu wakikatiza safari zao. Kwa sasa nimefunga hoteli yangu,” akasema Bw Shee.

Bw Bakari Bunu ambaye ni nahodha wa boti za watalii eneo la Shella, alisema biashara imekuwa ikididimia kila siku.Bw Bunu alisema wateja wao wengi huwa ni watalii kutoka ng’ambo.

Alieleza kuwa kwa sasa watalii wanaotegemea kuendesha biashara zao ni wale wa ndani kwa ndani kwani wale wa kimataifa wamesita kuingia nchini na kufika Lamu kujivinjari.

“Tumesalia kutegemea wageni kutoka Nairobi, Mombasa, Malindi na sehemu zingine za Kenya. Watalii wa ng’ambo wamesalia katika mataifa yao, ikizingatiwa kuwa siasa za uchaguzi wa Agosti 9 zinazidi kupamba moto nchini,” akasema Bw Bunu.

Bw Mohamed Omar ambaye hutoa huduma za kutembeza watalii ufuoni, alieleza kuwa kwa karibu mwezi mmoja, hajapata biashara.

Bw Omar alilaumu serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kwa kutelekeza sekta ya utalii na badala yake kuelekeza nguvu nyingi kwenye siasa.

Aliomba serikali kupitia wizara husika ya utalii nchini kuzingatia kuvumisha utalii wa Lamu na Kenya kwa ujumla kwenye mataifa ya nje.

“Wameelekeza nguvu nyingi kwa kampeni za kisiasa uchumi ukiendelea kuzorota. Wafikirie pia kurusha matangazo ya kuuza utalii wa Kenya ng’ambo. Wakiendeleza kutusahau hivyo tutaumia,” akasema Bw Omar.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Kaunti ya Lamu (LTA), Bw Ghalib Alwy, aliwarai wanasiasa na Wakenya kwa jumla kudumisha amani kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Sekta kama vile utalii na biashara hufanya vyema zaidi pahali ambapo kuna amani na utulivu. Wosia wangu kwa wanasiasa wetu na wakenya kwa jumla, tudumishe amani ili utalii na sekta nyingine zinoge na kuboresha uchumi nchini mwetu,” akasema Bw Alwy.

Hali sawa na hii ilianza kukumba pia sekta nyingine zinazotegemea masoko ya kimataifa ikiwemo uchukuzi wa mizigo bandarini.

  • Tags

You can share this post!

Wauzaji walalama kwa kukosa biashara kongamano la Kisumu

Serikali kubuni kanuni mpya za kuimarisha uvuvi

T L