Habari

Wito serikali isaidie shule kutimiza masharti

October 6th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

WADAU mbalimbali wa elimu nchini wameitaka serikali kuzisaidia shule kutimiza masharti kuhusu udhibiti wa maambukizi ya virusi vya corona, ili kuhakikisha wanafunzi wako salama wanaporejea shuleni wiki ijayo.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha amesema Jumanne wanafunzi wa Darasa la Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne watarejea shuleni Jumatatu wiki ijayo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, waziri amesema alichukua hatua hiyo kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta na mashauriano kati ya wadau wakuu wa elimu nchini.

Kwenye tangazo hilo, Muhula wa Pili utaanza Jumatatu na kudumu kwa wiki 11, hadi Desemba 23, 2020.

Baada ya hapo, wanafunzi wataanza likizo yao Desemba 24 hadi Januari 1, 2021. Hili linamaanisha kuwa wanafunzi watakuwa likizoni kwa wiki moja pekee.

Muhula wa Tatu utaanza Januari 4, 2021, hadi Machi 19, 2021.

Wanafunzi wa Darasa la Nane watafanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) kati ya Machi 22 na 24, 2021, huku wenzao wa Kidato cha Nne wakifanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) kati ya Machi 25 na Aprili 16, 2021.

Kwa mujibu wa waziri, mitihani hiyo itasahihishwa kati ya Aprili 19 hadi Mei 07, 2021.

Kwenye tangazo hilo, waziri aliwaagiza wasimamizi wote wa shule kuhakikisha wanazingatia masharti yote kuhusu udhibiti wa corona.

“Ni lazima watu wote wanaoingia shuleni wazingatie kanuni zote kuhusu udhibiti wa maambukizi ya corona kama vile uvaaji barakoa, kupimwa viwango vya joto, kuoshwa mikono na kuzingatia viwango vya juu vya usafi,” akasema Prof Magoha.

Licha ya tangazo hilo, wadau mbalimbali waliiagiza serikali kutoa fedha kuzisaidia shule kutimiza baadhi ya masharti hayo.

Sasa Chama cha Walimu wa Vyuo Anuwai (KUPPET), Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA) na Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA), wanairai serikali kushirikiana vilivyo na wazazi ili kuwaondolea wasiwasi ambao baadhi yao wamekuwa nao.

“Tunaunga mkono hatua ya serikali kufungua upya shule, kwani inalingana na baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Ufunguzi wa Shule (NERC). Hata hivyo, tunaiomba kutoa fedha kwa shule ili kuzisaidia kutekeleza masharti hayo,” akasema Katibu Mkuu wa KUPPET, Akelo Misori.

Mwenyekiti wa NPA, Bw Nicholas Maiyo, aliwaomba wazazi kuondoa wasiwasi wowote kuhusu usalama wa watoto wao, badala yake akiwaomba kushirikiana vilivyo na serikali.

“Badala ya kuendelea kuwa wenye wasiwasi, njia ya pekee ambapo wazazi wataisaidia serikali ni kushirikiana nayo kwenye utekelezaji wa masharti hayo,” akasema Bw Maiyo, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Wakenya mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter pia walieleza kuridhishwa kwao na uamuzi huo.