Wito serikali itoe sodo bila malipo

Wito serikali itoe sodo bila malipo

Na Maureen Ongala

MASHIRIKA ya kijamii ya katika kaunti ya Kilifi, jana walitaka serikali kuu kutoa sodo bila malipo kama vile inatoa mipira ya kondomu bure.

Kulingana na mashirika hayo, wanawake wengi mashinani wamekuwa wakikosa pesa za kununua sodo kwa sababu ya umasikini.

Wakiongozwa na msimamizi wa mradi katika shirika la Center for Rights Education and Awareness (CREAW) kaunti ya Kilifi, Faith Tsuma linalopigania haki za wanawake na wasichana nchini, na mkurugenzi wa shirika la Connect to Retain Nasim Jahangir, wanaitaka serikali kuwapatia sodo wasichana walioko shuleni na hata wale ambao hawaendi shule na wanawake pia.

Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha siku ya hedhi ulimwengini katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi, Bi Tsuma alisema serikali imeipa kipaumbele masuala ya ngono ambayo sio lazima kwa binadamu.

“Inasikitisha kwa sana kwa sababu kuwa kondomu zapatika bure na sodo hapana. Tunasema ngono sio shughuli ambayo ni ya lazima kwa binadamu kuifanya kila wakati, lakini kila siku wanawake na wasichana hupata siku zao za hedhi,” akasema.

Bi Tsuma alieleza masikitiko yake kuwa serikali kuu imewabagua wasichana ambao hawako shuleni katika mipango yao ya kuwapa sodo ilhali wao pia wanateseka vijijini kufuatia umaskini ambao unazidi kukithiri miongoni mwa jamii.“Kuna umuhimu wa serikali kuu kuhakikisha ya kwamba kila msichana anapata sodo ,” akasema.

Serkali kuu inatekeleza mpango wa kuwapatia wasichana wa shule sodo kupitia hazina ya National Government Affirmative Action Fund (NGAAF) inayoongozwa na wawakilishi wa wanawake katika kaunti zote 47 nchini.

Hata hivyo, Bi Tsuma aliendelea kusema kuwa sodo hizo huwa chache ikilinganishwa na uhitaji wa baadhi ya wasichana ambao huchukua zaidi ya wiki moja wakiwa katika siku zao za hedhi. “Wasichana wana hedhi tofauti na unapata kuwa pakiti mbili za sodo hazitawafaa baadhi yao,” akasema.

Pia, aliomba serikali kuongeza idadi ya sodo katika shule ili kumfaa kila msichana.Bi Yasin Jahangir wa Connect to Retain alisema kuwa suala la serikali kupeana mipira ya kondomu bure na kuuza sodo limewaudhi vijana wengi.

Alisema licha kuwa sodo zinauzwa mbei yake pia ni ghali na wanawake na wamama kutoka katika familia maskini hawana uwezo wa kununua.

“Umakini umekithiri mashinani hasa mashinani na unapata wasichana wanatumia njia mbadala ambazo sio katika njia ya usafi na zinahatarisha afya yao,”akasema.

Alisema kuwa baadhi ya wasichana kutoka jamii maskini wanalazimika kuchimba mashimo na kuketi hapo hadi siku watakapo maliza siku zao za hedhi.

Bi Jahangir alisema kuwa hatua ya jamii na serikali kutozungumzia kwa uwazi maswala ya hedhi imechangia kuwepo kwa matatizo mengi yanawakumba wanawake na wasichana.

You can share this post!

Ruto kuteua mwaniaji mwenza bila kushauri viongozi wa UDA

Kampuni yagundua kiwango kikubwa cha dhahabu